Malawi yajiandaa kutoa vikosi vyake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Malawi imetangaza kuwa inajiandaa kutoa vikosi vyake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limelizindua shambulizi jipya. 

Ofisi ya Rais ilisema kuwa vikosi hivyo vilikuwa sehemu ya ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliopelekwa mwaka 2023 kusaidia serikali ya Kinshasa kudhibiti machafuko katika kanda ya mashariki yenye rasilimali nyingi za madini.

“Rais (Lazarus) Chakwera ameamuru Kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Malawi kuanza maandalizi ya kutoa vikosi… ili kuheshimu tamko la kusitisha mapigano,” ilisema ofisi ya Rais Chakwera jioni ya Jumatano.

Hatua hii pia ni kwa ajili ya kuruhusu “mazungumzo yaliyopangwa kuelekea amani ya kudumu,” iliongeza taarifa hiyo.

Haikufahamika mara moja vikosi vitaanza lini kutoa sehemu ya vikosi vyao.

Afrika Kusini inaongoza kikosi cha SADC, kinachokadiriwa kuwa na wanajeshi takribani 1,300, huku Tanzania ikichangia wanajeshi pia.

Jumanne, kundi la M23 lilitangaza kusitisha mapigano kwa hiari huku likishinda mji wa Goma, ulio kaskazini mwa Kivu, lakini mapigano makali yalizuka asubuhi ya Jumatano, kati ya M23 na washirika wake wa Rwanda dhidi ya wanajeshi wa Kongo.

Vikosi vya M23 na wanajeshi wa Rwanda viliteka mji wa Nyabibwe, mji wa uchimbaji madini ulio takribani kilomita 100 (maili 60) kutoka Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, na kilomita 70 kutoka uwanja wa ndege wa jimbo hilo.

Viongozi kutoka jumuiya ya nchi 16 za SADC na jumuiya ya nchi 8 za Afrika Mashariki wanatarajiwa kukutana Jumamosi, katika juhudi za kufanikisha amani kati ya pande zinazohasimiana nchini DRC.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo nchini Tanzania baada ya kutokuwepo katika mazungumzo ya awali.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kuendesha kikao cha dharura kuhusu mgogoro wa DRC Ijumaa.

Angalau watu 900 walikufa katika mapigano ya Goma na 2,880 walijeruhiwa, kulingana na shirika la misaada la Umoja wa Mataifa.

Waangalizi wa kimataifa wametahadharisha kuhusu dharura ya kimaisha inayoweza kutokea mashariki mwa nchi hiyo.