Malipo ya fidia kwa waathirika wa ajali ya ndege kufanyika kwa siri

Mkurugenzi wa Shirika Precision Air, Patrick Mwanri amesema mchakato wa malipo ya fidia kwa familia zilizoathiriwa na ajali hiyo tayari umeshaanza ambapo utakuwa kati ya familia za waliothirika na shirika hilo na utakuwa wa siri na utafanyika kwa umakini mkubwa.

Kauli ya Mwanri inakuja zikiwa zimepita takribani siku saba tangu kutokea kwa ajali ya ndege ya shirika hilo iliyosababisha vifo 19 na majeruhi 24.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 14 Mwanri amesema, shirika hilo lina bima inayolingana na taratibu za uendeshaji wa mashirika ya ndege.

“Shirika letu lina bima na ipo kulingana na taratibu za uendeshaji mashirika ya ndege. Hivi ninavyoongea taratibu zile zimeshaanza na wahusika tumeshaanza kuwasiliana nao ili waweze kupata taarifa rasmi ya nini kinahitajika”– amesema Mwanri na kuongeza 

“Mara nyingi suala hili hufanyika kwa faragha kati ya wahusika na sisi hatutalileta hadharani.Tuna mawasiliano ya karibu na majeruhi wote tangu wakiwa hospitali hata baada kutoka tukiwasaidia kwa namna mbalimbali kadiri ya uwezo wetu,”.

Pamoja na hilo Mwanri amesema shirika hilo lilichukua jukumu la kusafirisha miili yote kulingana na matakwa ya familia husika zilizopatwa na misiba.

Wakati wa shughuli ya kuaga miili hiyo mkoani Kagera, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali itasimamia gharama za mazishi na kuagiza wakuu wa Mikoa ambapo miili hiyo itapelekwa wasimamie zoezi hilo kikamilifu.

Ndege hiyo ilianguka katika Ziwa Victoria takribani mita 100 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, mkoani Kagera ikiwa na watu 43 waliokuwa wakitoa jijini Dar es Salaam, kati yao 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.

Baada ya ajali hiyo iliyotokea Novemba 6, mwaka huu saa 2:53 asubuhi, shughuli za uokoaji kwa sehemu kubwa zilifanywa na wavuvi wakiongozwa na kijana Jackson Majaliwa na wenzake waliowezesha watu 24 kuokolewa.

https://mwanzotv.com/2022/11/07/tanzania-yatuma-risala-za-rambirambi-kwa-waathiriwa-wa-ajali-ya-ndege/