Mali:Wanajeshi 27 wauawa katika shambulio la wanajihadi

Shambulio la wanajihadi kwenye kambi ya kijeshi katikati mwa Mali siku ya Ijumaa liliua wanajeshi 27 ,jeshi la nchi hiyo lilisema.

Mapigano hayo yalisababisha wanajeshi 33 kujeruhiwa, 21 vibaya, na saba hawajulikani walipo, jeshi liliongeza katika taarifa yake.

Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa likipambana na vuguvugu la wanajihadi lenye mafungamano na Al-Qaeda na kundi la Islamic State kwa takriban muongo mmoja.

Chanzo cha jeshi la Ufaransa kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kilisema mamia ya wanajihadi walishambulia kambi ya wanajeshi 150 mwendo wa saa 0600 GMT, na kuongeza idadi ya waliouawa kuwa kati ya 40 na 50. Jeshi la Mali lilisema shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa 0530 GMT.

Wanajihadi hao waliteka magari 21, vikiwemo vifaru, na kuwajeruhi zaidi ya wanajeshi 20, chanzo hicho kiliongeza.

Chanzo hicho kilisema kuwa jeshi la Mali halikuomba kuungwa mkono na operesheni ya kijeshi ya Ufaransa ya Barkhane kwa sababu kambi hiyo “ndipo Barkhane aliombwa asifanye kazi, pengine kwa sababu ya kuwepo kwa mamluki wa Wagner” akimaanisha kundi la wanamgambo wa Urusi.

Afisa wa kijeshi aliiambia AFP jeshi na jeshi la anga “lilichukua hatua kali”.

Kambi ya Mondoro iko karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso na hapo awali imekuwa ikilengwa na wanajihadi wanaopigana na serikali ya Mali na vikosi vya kigeni.

Takriban wanajeshi 50 walikufa baada ya shambulio la Mondoro na kambi ya karibu ya Boulkessi mnamo Septemba 2019.

Jeshi la Ufaransa limesema takriban washambuliaji 100 ‘walifurushwa’ kufuatia juhudi kati ya Barkhane na jeshi la Mali dhidi ya wanajihadi waliojaribu kuteka kambi hiyo Januari 2021.

Wanajihadi na wapiganaji wanaotaka kujitenga — baadhi wakiwa na mfungamano na Al-Qaeda na kundi la Islamic State — walianza operesheni nchini Mali mwaka 2012 na mzozo huo umeenea hadi nchi jirani za Niger na Burkina Faso, na kuua na kuwafukuza maelfu ya raia.

Shambulio la Ijumaa limetokea wakati hali ya kijeshi katika eneo hilo ikibadilika kufuatia uamuzi wa Ufaransa kujiondoa kutoka Mali na kuwasili kwa wakufunzi wa Urusi, ambayo nchi za Magharibi zinasema ni mamluki wa Wagner.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya utawala wa kijeshi wa Bamako na Paris umezorota katika miezi ya hivi karibuni huku jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi ikiweka vikwazo vikali kwa serikali ya Mali kuchelewa kurejea katika utawala wa kiraia.