Malori nchini Tanzania sasa kuwekewa vidhibiti mwendo

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kuanzia sasa mabasi na malori yanatakiwa kufungwa vidhibiti mwendo ili kuzuia ajali.

Alitoa maagizo baada ya  kikao kilichohusisha viongozi wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani cha kujadili na kushauriana namna bora ya kudhibiti ajali za barabarani.

Masauni alisema anatoa maelekezo matano likiwemo la mabasi na malori na akasema kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani vyombo hivyo vya usafiri vinatakiwa kufungwa vidhibiti mwendo.

“Naagiza jambo hilo lishughulikiwe na watakaokiuka wapelekwe mahabusu na mahakamani, serikali haiwezi kuona watu wanateketea, hatukubali,” alisema.

Katika kuhakikisha hilo linatekelezwa Masauni ametoa miezi sita kwa waliochezea mfumo huo wawe wamerekebisha ili kusiwe na kisingizio chochote baada ya muda huo kupita.

Masauni alisema Jeshi la Polisi litaanza operesheni maalumu za usalama barabarani kwa lengo la kudhibiti ajali.

“Imefika wakati wa kupitia upya utoaji wa mafunzo ili Jeshi la Polisi likague vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya udereva ili madereva wanapotoka chuoni wawe wameiva na anatambua dhamana ya kazi yake,” alisema.

Aliwataka madereva na wamiliki wa magari wawe makini ili kuzuia ajali kama iliyotokea Machi 28 mwaka huu wakati kontena lilipoangukia gari dogo na kuua watu wawili eneo la Mlandizi mkoani Pwani.

Masauni alisema utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulibaini asilimia 76 ya vyanzo vya ajali vinatokana na sababu za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuendesha kwa mwendo unaozidi uliowekwa kisheria au dereva kuendesha akiwa amelewa pombe.