Mamlaka ya Mawasiliano Kenya yapiga “Stop” vyombo vya habari kurusha “Live”maandamano

 Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imeamuru vituo vyote vya televisheni na redio kusitisha mara moja matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yanayoendelea kote nchini, hatua iliyozua hisia kali kutoka kwa watetezi wa haki za habari, viongozi wa upinzani, na wanaharakati wa kiraia.

Agizo hilo, lililotolewa rasmi leo Juni 25, 2025, linanukuu madai ya ukiukaji wa Kifungu cha 33(2) na 34(1) cha Katiba ya Kenya, pamoja na Kifungu cha 461 cha Sheria ya Mawasiliano na Habari ya Kenya (Kenya Information and Communications Act).

Kwa mujibu wa CA, matangazo ya moja kwa moja “yanahatarisha usalama wa taifa, kuchochea chuki na uvunjifu wa amani,” hasa katika kipindi hiki ambapo maelfu ya Wakenya  wengi wao wakiwa vijana wa kizazi cha Gen Z wamejitokeza mtaani kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano makali dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2024 yaliyopelekea vifo vya watu kadhaa.

 

CA YATISHIA HATUA ZA KISHERIA KWA WASIOZINGATIA AGIZO HILO

Katika taarifa yake, CA imeonya kuwa vyombo vya habari vitakavyokiuka agizo hilo vitakabiliwa na hatua kali za kisheria na kisheria.

“Vyombo vya habari vina wajibu wa kuheshimu mipaka ya uhuru wa kujieleza, hasa inapohusisha masuala yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya mamlaka hiyo.

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa vikali na wanahabari na mashirika ya kutetea haki za kiraia, wakisema kuwa ni jaribio la wazi la kufifisha sauti ya wananchi na kupunguza uwazi kuhusu yanayojiri katika maandamano ya kitaifa.

Maandamano ya leo yamefanyika kote nchini huku waandamanaji wakilalamikia kupanda kwa gharama ya maisha, ushuru wa juu, na ukosefu wa ajira kwa vijana.

Hali ya taharuki imeshuhudiwa katika baadhi ya maeneo huku polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi na kuweka vizuizi katika barabara kuu. Watu kadhaa wamejeruhiwa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na ya kijamii wameeleza hofu kuwa hatua hiyo ni dalili ya kushuka kwa kiwango cha demokrasia na uwazi nchini Kenya, huku sauti ya wananchi ikizidi kuzimwa kupitia njia za kisheria.

Shirika la Amnesty International liliungana na wakosoaji wengine kulaani marufuku hiyo, likisema kuwa:

“Kuwanyamazisha wanahabari si suluhisho. Uhuru wa habari ni msingi wa demokrasia na haki za binadamu.”

 

WAKENYA WATILIA SHAKA AGIZO HILO, BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI VYAENDELEA KURUSHA MATANGAZO

Agizo hilo la CA lilikumbana na upinzani mkali mtandaoni, ambapo wananchi wengi walieleza hasira na hofu kuwa serikali inalenga kuficha ukweli wa yanayojiri.

Licha ya agizo hilo, vyombo vingi vya habari nchini viliendelea na matangazo ya moja kwa moja. The Standard Group ambayo inamiliki runinga, redio na gazeti  ilitoa taarifa ikilaani hatua hiyo, ikiitaja kuwa ni jaribio la “kuzima habari.”

“Tuna taarifa kwamba CA imewaagiza wasambazaji wa mitandao ya matangazo kuziondoa hewani taasisi yoyote ya habari inayorusha maandamano moja kwa moja,” ilisema Standard Group.

Kampuni hiyo pia ilifichua kuwa vitisho kama hivyo vilitolewa wakati wa maandamano ya 2024, na kwamba haitatishika wala kusitisha kazi yake ya kuwahabarisha wananchi.