Maono ya  Zuhura Yunus Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Tanzania

Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Tanzania

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus ametaja vipaumbele vyake kuwa ni kukuza mawasiliano ya taasisi hiyo ya Ikulu, wizara za serikali na waandishi wa habari.

Akizungumza katika mahojiano maalumu baina yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Zuhura alisema ana uhakika ataimudu nafasi hiyo licha ya changamoto zitakazokuwepo  na kwamba jambo muhimu ni kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano.

“Pale (Ikulu) ilikuwa kupata watu kuzungumza na sisi (waandishi wa habari) ilikuwa ni mtihani na wakati mwingine unakuta labda taarifa wanazo lakini hawajui jinsi gani ya kuzitoa.

“Jambo kubwa ni kuweka muungano mzuri baina ya Rais Samia Ikulu na wizara zake na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa ili kuwe na hali nzuri ya kuwasiliana,” alisema Zuhura.

Kuhusu kupata uteuzi wa nafasi hiyo Zuhura  alisema alipata taarifa kuhusu uteuzi kupitia ujumbe mfupi na simu kutoka kwa marafiki zake, lakini katika maisha yake hakuwahi kufikiria kuwa atakuja kufanya kazi na serikali hasa katika nafasi nyeti

“Nilikuwa nimelala kawaida mie simu yangu kweli huwa nawasiliana na watu wengi kwa Whatasapp.Sasa nimeamka nakuta simu za kawaida zimepigwa si kawaida, nikashangaa mbona kuna watu kadhaa wamenipigia na hawana desturi ya kunipigia simu na mie mara nyingi nikiona simu kama hizo nawaza kifo,” alisema Zuhura.

Alisema baada ya kujihoji ilibidi ajipe ujasiri angalau kwa sekunde mbili na akapokea simu kutoka kwa rafiki yake anayeishi Tanzania ambaye baada ya kupokea tu alipiga kelele za kumpongeza.

“Nilipoipokea tu ile simu nikaona anapiga kelele hongeraaaa nikashangaa.

Ikabidi niingie Whatsapp kuona kwani kuna nini ndio sasa nikakuta nimeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu,” alisema Zuhura 

“Najua changamoto zitakuwepo lakini nitaimudu hii nafasi. Muda wote ambao nimefanya kazi ya uandishi wa habari kuna hali fulani ya kuheshimiana.

Hakika mahusiano hayakuwa mabaya sana zipo changamoto ambazo tumezishuhudia lakini kwa ujumla mambo yatakuwa mazuri,” alisema Zuhura.

Pamoja na yote Zuhura bado anaikumbuka ofisi yake ya zamani BBC kwa mambo mengi kwa kuwa imemkuza katika nyanja nyingi hasa za kimataifa.

“Mimi hapa Zuhura Yunus BBC imenilea na nimepitia katika mikono mingi kwa kuwa nilianza BBC redio mpaka nikaja televisheni,” alisema.

Zuhura Yunusi ni moja ya wanawake wanaoingia kwenye historia mbalimbali za kiutendaji, kwani yeye ndiye mwanamke wa kuwanza kutangaza kipindi cha dira ya dunia kinachorushwa na BBC, lakini pia ni mwanamke wa kwanza nchini Tanzania kushikilia nafasi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu.

Februali Mosi ndio historia hiyo iliandikwa baada ya Rais Samia Suluhu Hasaan kufanya mabadiliko katika nafasi hiyo nyeti, ambapo awali ilikuwa ikishikiliwa na Jaffar Haniu ambaye sasa amepangiwa kazi nyingine.