Watu wawili wamekamatwa siku ya Jumatano baada ya kupanda hadi kwenye mnara wa antena uliopo juu ya Jengo la Empire State jijini New York, Marekani, huku ikionekana kuwa walifanya tukio la uchumba wakiwa huko.
Wapenzi hao, waliokuwa wamevaa mavazi meusi na kufunika nyuso zao, walitundika bango juu ya jengo hilo lenye urefu wa futi 1,454 (mita 443) lililoandikwa
“Pale ambapo nguvu ya upendo inashinda tamaa ya madaraka, dunia hujua amani.”
Msemaji wa Polisi wa New York aliliambia shirika la habari la AFP kwamba watu hao wawili walikamatwa bila kutokea vurugu yoyote.
“Hakuna mtu aliyejeruhiwa. Uchunguzi bado unaendelea na mashtaka dhidi yao bado hayajatangazwa,” alisema msemaji huyo.
Baada ya kufika juu ya jengo hilo, mwanaume huyo alipiga goti moja chini na kuonekana akimvisha au kumposa mpenzi wake kabla ya wawili hao kubusiana na kukumbatiana.
Jengo la Empire State lina sehemu maalumu ya kutazamia mandhari ya Jiji la New York ambayo iko wazi kwa umma. Hata hivyo, maeneo ya juu zaidi ya jengo hilo hayaruhusiwi kufikiwa na wageni.
Licha ya marufuku hiyo, kumekuwa na watu waliowahi kujaribu kupanda jengo hilo hapo awali. Haikufahamika mara moja jinsi wapenzi hao walivyofanikiwa kufika kwenye antena ya juu ya jengo hilo.