
Marekani na Iran zimetangaza kufikia makubaliano ya kusitisha vita vya Mashariki ya Kati katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon, pamoja na kufungua tena Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani. Hata hivyo, pande hizo hazijatoa ufafanuzi wa kutosha kuhusu suala nyeti la mpango wa nyuklia wa Tehran.
Washington na Islamabad zimesema makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini Ijumaa nchini Uswisi, hatua inayotazamwa kama mafanikio makubwa katika juhudi za kumaliza miezi kadhaa ya vita vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuyumbisha masoko ya nishati duniani.
Ingawa maelezo kamili ya makubaliano hayo bado hayajawekwa wazi, Rais wa Marekani Donald Trump amesema Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani, utafunguliwa tena mara baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo.
“Makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa yamekamilika,” Trump aliandika katika mitandao ya kijamii jana Jumapili wakati akisherehekea miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
“Vyombo vya usafiri wa majini duniani viendelee na safari. Mafuta yaruhusiwe kutiririka tena,” aliongeza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema makubaliano hayo yanamaliza mara moja vita kati ya nchi hizo mbili na kwamba mazungumzo zaidi yatafanyika ndani ya miezi miwili ijayo kwa lengo la kufikia makubaliano ya mwisho.
Awali, Tehran ilikuwa imetishia kulipiza kisasi kufuatia shambulio la Israel dhidi ya kundi la Hezbollah katika viunga vya Beirut, tukio lililoonekana kuhatarisha juhudi za kufikia makubaliano hayo.
Baadaye, Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alitangaza kuwa pande zote mbili zimekubaliana kusitisha mara moja na kwa kudumu operesheni za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon.
Sharif pia aliwashukuru viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na Uturuki kwa mchango wao katika juhudi za upatanishi.
-Maelezo Bado Hayajawekwa Wazi-
Yaliyomo katika makubaliano hayo bado hayajafafanuliwa kikamilifu. Hata hivyo, Shirika la Habari la Mehr la Iran limeripoti kuwa Marekani imekubali kuachia sehemu ya mali za Iran zilizokuwa zimezuiwa nje ya nchi kabla ya kuanza kwa mazungumzo rasmi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makubaliano ya awali yana vipengele 14, ikiwemo kuachiliwa kwa mabilioni ya dola za mali za Iran zilishikiliwa katika kipindi cha siku 60 za mazungumzo.
Utawala wa Trump haujatoa tamko rasmi kuhusu maelezo hayo. Moja ya masuala yanayoendelea kujadiliwa ni mpango wa nyuklia wa Iran na hatma ya akiba yake ya urani iliyoboreshwa kwa kiwango cha juu.
Katika mahojiano na gazeti la New York Times, Trump alisema bado kuna mazungumzo kuhusu uwezekano wa Iran kusitisha shughuli za urutubishaji wa urani kwa miaka 20, ingawa alidokeza kuwa muda wa miaka 15 unaweza pia kuzingatiwa.
Jumuiya ya Kimataifa Yakaribisha Hatua Hiyo-
Tangazo la makubaliano hayo limepokelewa kwa matumaini makubwa na jumuiya ya kimataifa.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua hiyo ni muhimu katika juhudi za kumaliza vita vya Mashariki ya Kati.
Nchi za Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia zimetangaza kuwa ziko tayari kuondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran na kushirikiana na Marekani pamoja na washirika wa kikanda kuhakikisha mchakato huo unafanikisha suluhisho la kudumu la kidiplomasia.
Masoko ya kimataifa pia yameonyesha ishara za nafuu kufuatia tangazo hilo. Bei za mafuta zilishuka kwa zaidi ya asilimia nne katika soko la Tokyo, huku faharasa ya hisa ya Nikkei nchini Japan ikipanda kwa asilimia tatu.
Kwa miezi kadhaa, kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kulikuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na kuathiri minyororo ya usambazaji wa bidhaa muhimu, ikiwemo mbolea zinazotumika katika uzalishaji wa chakula.
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema kufunguliwa kwa njia hiyo kutasaidia kupunguza gharama za nishati kwa muda mfupi na mrefu na kuchochea ustawi wa kiuchumi katika Mashariki ya Kati.
-Shambulio la Israel Lilitikisa Mazungumzo-
Jumapili ilishuhudia mvutano mkubwa baada ya Trump kuilaumu Israel kwa kuchelewesha kukamilika kwa makubaliano hayo kufuatia shambulio la anga lililolenga viunga vya Beirut.
Katika mahojiano na chombo cha habari cha Axios, Trump alionyesha kutoridhishwa kwake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akisema alikasirishwa na hatua hiyo na kumweleza wazi msimamo wake.
Mara ya mwisho Israel iliposhambulia maeneo ya Beirut, hali hiyo ilisababisha kuongezeka kwa mvutano baada ya Iran kujibu kwa mashambulizi ya makombora, huku Israel nayo ikijibu kwa mashambulizi mengine.
Kwa muda mrefu Iran imekuwa ikisisitiza kwamba makubaliano yoyote ya kusitisha vita lazima yajumuishe pia mzozo wa Lebanon, ambako Israel imekuwa ikiendesha operesheni za kijeshi dhidi ya Hezbollah inayoungwa mkono na Tehran.