Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umeungana na raia wengine wa taifa hilo kushtumu mauaji ya mwanasiasa wa chama cha upinzani Chadema Ali Mohammed Kibao.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kupitia mtandao wa X zamani Twitter, Ubalozi huo sasa unaitaka serikali kufanya uchunguzi huru na ulio wazi kuhusu utekaji wa watu na mauaji ya mwanasiasa huyo wa Chadema.
Umesisitiza kwamba mauaji pamoja na utekaji ni masuala ambayo hayafai kuwa na nafasi katika demokrasi ya taifa hilo.
‘Mauaji pamoja na kupotea kwa watu, pamoja na kukamatwa , kupigwa na juhudi zengine za kuwaengua raia katika uchaguzi uliotokea mwezi uliopita havipaswi kuwa na nafasi katika demokrasia’, ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongezea kwamba vitendo hivi vya kikatili vinadhoofisha haki zinazohakikishiwa na katiba ya Tanzania.
Ubalozi huo umetuma rambirambi zake za dhati kwa familia ya bwana Kibao na kwa taifa kwa kupoteza maisha yake na uongozi wake wa kiraia.
Matukio ya utekaji yamekua yakiripotiwa kwa wingi katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa katibu wa Chadema John Mnyika ,Mzee Ali kibao alikua safirini kuelekea mkoani Tanga kabla ya kuchukuliwa na watu wenye silaha na pingu kisha kumshusha kwa nguvu.
‘’Jana majira ya saa 12 jioni lilitokea tukio ninaliita la kutekwa siyo kukamatwa kwa Mzee Ali Mohamed Kibao ambaye ni mjumbe wa Sekretariati ya Chadema taifa, tukio hilo limetokea maeneo ya Kibo karibu na Tegeta, Mzee Kibao akiwa anasafiri kutoka Dar es salaam kwenda Tanga, basi hilo lilizuiwa na gari mbili, walishuka watu wakiwa na silaha na kumwambia dereva asiondoe basi, kisha kwenda kwenye kiti alichokaa na kumchukua kwa nguvu” Alisema Mnyika’’.
Ali Kibao amezikwa leo, nyumbani kwake mkoani Tanga, ambapo viongozi mbalimbali wa kisiasa wamehudhuria katika mazishi hayo