Martha Karua: Kenya iko katika hali ya siasa na uchumi isiyovumilika

Mwanasiasa mkongwe Martha Karua ametangaza nia yake ya kugombea urais wa Kenya katika uchaguzi wa mwaka 2027, akisema kuwa nchi hiyo iko “katika hali ya vurugu kamili” kutokana na ufisadi, mauaji yanayotekelezwa na polisi, na kuzorota kwa uchumi.

Karua amesema kuwa hali ya sasa ni kama vile katiba ya nchi imesimamishwa. “Tuko katika vurugu kamili. Ni kana kwamba katiba yetu imesitishwa,” alisema. “Kuna utekaji nyara, kukamatwa kiholela… mauaji ya kiholela… na polisi pamoja na mamlaka hawawajibiki.”

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuwa watu wasiopungua 60 waliuawa wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko la ushuru na ufisadi mwezi Juni na Julai mwaka jana, huku wengine 89 wakitekwa nyara, na 29 bado hawajulikani waliko.

Karua, ambaye aliwahi kuwa waziri wa sheria katika serikali ya marehemu Rais Mwai Kibaki, aliondoka serikalini mwaka 2009 akilalamikia wenzake waliokuwa wakipinga mageuzi. Tangu hapo, amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanasiasa wa upinzani waliokamatwa katika nchi jirani kama Tanzania na Uganda.

Katika uchaguzi wa 2022, Karua aligombea nafasi ya makamu wa rais akiwa mgombea mwenza wa Raila Odinga. Sasa, anaungana na viongozi wengine wa upinzani kujipanga kwa uchaguzi ujao.

Karua alisema kuwa kipaumbele chake cha kwanza iwapo atachaguliwa kuwa rais ni kufunga mianya ya upotevu wa fedha na kuleta nidhamu ya kifedha, kwani Kenya inakabiliwa na deni la zaidi ya dola bilioni 85 za Kimarekani. “Kupambana na ufisadi ndiyo njia pekee ya kuokoa nchi hii,” alisema. “Bila hivyo, tutapoteza kila tunachokusanya au kukopa, na hatutawahi kuwaondoa Wakenya kwenye mateso yao.”

Ingawa sasa anashirikiana na baadhi ya wanasiasa wa upinzani wenye historia ya utata, Karua alisema kuwa kuiondoa serikali iliyoko madarakani ni kazi kubwa inayohitaji ushirikiano wa kila mtu. “Jukumu la kuiondoa serikali isiyofuata sheria ni kazi kubwa. Tunahitaji mikono yote,” alieleza.

Hata hivyo, alionya kuwa uchaguzi wa 2027 unaweza kushuhudia machafuko na udanganyifu. Akitaja historia ya uchaguzi wa 2007 uliogubikwa na vurugu, ambapo Rais Ruto alishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kabla kesi hiyo kufutwa kwa kukosekana kwa ushahidi, Karua alisema kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi safari hii.

Alimshutumu Ruto kwa kuajiri vijana kufanya vurugu katika mkutano wake wa hivi karibuni jijini Nairobi, ambapo mashambulizi na wizi kwa raia viliripotiwa. “Najua hali itazidi kuwa mbaya. Watatumia fedha za umma kwa kampeni badala ya huduma muhimu kama afya, elimu na usalama,” aliongeza.

Msemaji wa ikulu alikanusha madai hayo, akisema kuwa “Ruto hajawahi kuajiri au kulipa watu kuhudhuria mikutano yake.” Aliongeza kuwa Karua na timu yake walitengeneza uongo kama huo wakati wa uchaguzi uliopita, na sasa wako njiani kupata kichapo kikubwa zaidi.

Licha ya changamoto hizo, Karua anasisitiza kuwa suluhisho pekee ni “wimbi kubwa la kura” ambalo haliwezi kupingwa kwa njia yoyote ya udanganyifu. “Njia pekee ya kushinda njama za Ruto ni kwa kuwa na idadi kubwa ya kura ambayo haiwezi kuchezewa,” alisema.