Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ametengeneza mazingira mazuri ya kisiasa na kuifanya nchi kuwa usalama, hivyo hakuna sababu za viongozi wa kisiasa ikiwemo wa chama cha Chadema, walioko uhamishoni kutorejea Tanzania.
Mojawapo ya viongozi wa kisiasa ikiwemo wa chama cha Chadema, walioko uhamishoni ni Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini Chadema, Godbless Lema (Canada) na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu (Ubelgiji).
Mhandisi Masauni ametoa kauli hiyo, bungeni jijini Dodoma, leo akimjibu Mbunge Viti Maalum, Grace Tendega, aliyetaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu viongozi wa Chadema, walioko nje ya nchi.
“Hakuna sababu yoyote kwa Mtanzania aliyeko popote pale ikiwemo viongozi hao wa Chadema, walioko nje ya nchi kutorejea nchini ili sio tu waweze kutumia fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi na kisiasa, lakini kushiriki kikamilifu katika kutoa michango yao kwa maendeleo ya nchi yao katika nyanja yoyote kwani hapa ni nyumbani kwao,” amesema Mhandisi Masauni.
Amesema, uthibitisho ya kwamba Rais Samia ameimarisha mazingira ya kisiasa, unaotokana na mwitikio mkubwa wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini, pamoja na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani, akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Babu Juma Duni Haji na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
“Nichukue fursa hii kulieleza Bunge kuwa, nchi yetu iko salama haina tishio lolote la kiusalama, wimbi la ongezeko kubwa sana la wawekezaji Watanzania na wageni ni uthibitisho wa mazingira mazuri ya kiuchumi na kisiasa yaliyoko nchini. Nataka nihakikishe kuwa Serikali ya Rais Samia itaendelea kuhakikisha kwamba hali ya kisiasa na kiuchumi iliyoko nchini inaendelea kudumu,” amesema Mhandisi Masauni.