Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, amesema kumekuwa na ushirikiano mdogo kwa waathiriwa wa utekaji pindi wanapohitajika na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kutoa ushirikiano utakaofanikisha upelelezi.
Masauni amezungumza hayo leo wakati akihojiwa na kituo cha habari cha Wasafi Tv, ambapo ametolea mfano sakata la kutekwa kwa Sativa hivi karibuni.
Waziri Masauni amedai kuwa Sativa hana ushirikiano mzuri kwa Jeshi la Polisi kuzungumzia yaliyomkuta hadi kupatikana mkoani Katavi.
Edgar Mwakabela (27) maarufu katika mtandao wa X (zamani Twitter) kwa jina la Sativa alitoweka Juni 23, 2024 baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana na alipatikana mkoani Katavi, Juni 27, 2024 akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter Sativa amekiri kufatwa na Polisi wakimtaka wafanye nae mahojiano ya kilichotokea lakini kutokana na hali yake ya kiafya kwa sasa kutokaa sawa imemlazimu kuwaambia polisi kwamba bado yupo kwenye matibabu.
Amedai kuwa tangu afanyiwe oparesheni Julai 2,2024 bado hajaweza kuzungumza vizuri.
“Kwa zaidi ya week 4 sasa tangu nimefanyiwa operation tarehe 2/7 siwezi kufungua mdomo. Hata ongea yangu ni ya shida, kuna maneno nikiongea huwezi kunisikia vizuri. Kucheka siwezi, kupiga chafya siwezi, kupiga mihayo siwezi”- Sativa kwenye ukurasa wake wa X
Aidha amesema pamoja na hayo alishahojiwa na Polisi mkoani Katavi kwa zaidi ya saa tatu hivyo ni suala ambalo Polisi wanalijua vizuri.