Mashine za kukusanyia mapato hazionekani kwenye mifumo

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini mashine 1,355 za kukusanyia mapato (POS) katika Mamlaka 46 za Serikali za Mitaa, kutoonekana katika mfumo wa kukusanyia mapato kwa kipindi cha kati ya siku tatu hadi siku 4,274 bila taarifa yoyote.

Pia alisema mwongozo wa usimamizi wa mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, unazitaka mamlaka hizo kutekeleza udhibiti wa ndani katika ukusanyaji wa mapato.

Hayo yamo katika ripoti kuu ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2020/21.

Kichere alisema udhibiti huo ni muhimu katika kuimarisha uwajibikaji, kulinda mapato yanayokusanywa, kuwapo kwa kumbukumbu sahihi za mapato, kuzingatia taratibu za ukusanyaji wa mapato na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Nilibaini mamlaka nane za Serikali za Mitaa zilikuwa na upotevu wa mashine 34 za POS, mamlaka 20 za Serikali za Mitaa zilikuwa na jumla ya walipa kodi 890 ambao walikuwa wamesajiliwa katika Mfumo wa Kukusanyia Mapato (LGRCIS) kwa namba ya utambulisho zaidi ya moja,” alisema Kichere.

Aliongeza: “Rejesta za POS katika mamlaka 14 za Serikali za Mitaa hazikuwa na taarifa za kutosha, hivyo kusababisha kutokuwapo taarifa muhimu kama vile majina ya wakusanyaji wa mapato ambao wamepatiwa mashine za POS na maeneo ambayo mashine za POS zinatumika.”

Kwa mujibu wake, mamlaka sita za Serikali za Mitaa hazikufanya usuluhishi wa taarifa za mapato kati ya mashine za POS, mfumo wa kukusanyia mapato na taarifa za benki, jambo ambalo ni kinyume cha mwongozo wa usimamizi wa mapato ya mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 unaotaka usuluhishi wa taarifa hizo walau kila wiki.

Alisema mashine za POS zilizopatikana kutoka Tamisemi katika kipindi cha mwaka 2018/19, hazioneshi namba ya utambulisho wa kifaa (IMEI) katika mfumo wa kukusanyia mapato.

Kichere alisema mashine hizo zilirekodiwa kwa namba ya utambulisho inayofanana ambayo ni -100, hivyo kusababisha ugumu katika kutambua kifaa halisi na kile ambacho kimerekodiwa katika mfumo.

Kutokana na mapungufu hayo, ameushauri uongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kuboresha udhibiti wa mashine za POS kwa kuhakikisha kila wakati taarifa inakuwapo kuhusu mashine za POS ambazo hazijaonekana katika mfumo kwa zaidi ya saa 48.

Hiyo ni ili kuondoa uwezekano wa upotevu wa mapato kutokana na mashine zinazokusanya mapato bila kuunganishwa katika mfumo wa kukusanyia mapato.

Pia aliishauri mamlaka hiyo kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu mashine za POS zilizopotea pamoja na kuondoa usajili wake katika mfumo wa kukusanyia mapato, kuondoa namba za utambulisho za wakusanyaji wa mapato ambao wamesajiliwa kwa namba zaidi ya moja na kuhakikisha kila mlipa kodi amesajiliwa kwa namba moja pekee.

Kichere pia alisema mamlaka ya Serikali za Mitaa inapaswa kuhakikisha usuluhishi wa taarifa za mapato unafanyika kila wiki ili kuondoa uwezekano wa kuwa na fedha nyingi za makusanyo ambazo hazipelekwi benki.