Matukio ya ubakaji yaongoza kwenye matukio ya ukatili nchini Tanzania

Serikali ya Tanzania imetaja jumla ya matukio 11,499 ya ukatili yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 huku ubakaji ukiongoza kwa idadi ya matukio hayo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu nchini Tanzania, Dk Doroth Gwajima amesema kuwa matukio ya ubakaji yaliripotiwa 5900 yakifuatiwa na mimba 1677 na ulawiti yalifikia 1474 lakini mengi yametajwa kuwa hayaripotiwi.

Dk Gwajima ametaja mikoa mitano inayoongoza kwa kiwango cha juu ukilinganisha na maeneo mengine ambayo ni Arusha, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Ilala.

Amesema Serikali ya nchi hiyo imejidhatiti kumaliza vitendo vya ukatili kwa kutoa adhabu kali kwa wahusika lakini akaomba ushirikiano uwe wa kutosha kwa kila Mtanzania ili kulinda watoto.

Hata hivyo Waziri Dk Gwajima amesema asimilia 60 ya ukatili unaoripotiwa unatokea majumbani wakati asilimia 40 ya taarifa za matukio inaripotiwa shuleni hivyo ameonya wanaohusika lazima washughulikiwe kwa nguvu ya pamoja.

“Lakini moja ya mambo tunayofanya sasa ni kufanya mapitio ya sheria ya mtoto ya mwaka 2019, hali si nzuri katika maeneo yote hivyo lazima tuunganishe nguvu ya pamoja na kutoa taarifa za vitendo hivyo,” alisema Dk Gwajima.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabil Shekimweri amekiri kuwa ukatili bado ni tatizo kwani hata Dodoma licha ya kutokuwa katika orodha ya mikoa ya juu kwenye ukatili, lakini hali siyo nzuri.