HalmashauriI ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imepiga marufuku uingizwaji wa nguruwe pamoja na matumizi ya mazao ya mnyama huyo kama nyama, damu, samadi, mifupa pamoja na nywele kutokanana na kubainika kwa uwepo ugonjwa wa homa ya nguruwe ndani ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Daktari wa Mifugo wa wilaya hiyo Festo Mkomba imesema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya hivi karibuni kujitokeza baadhi ya matukio yanayosababishwa na ugonjwa huo hivyo kwa mujibu wa sheria ya mifugo namba 16(2), 17 ya mwaka 2003 imembidi kutangaza kusitishwa kwa huduma hizo kuanzia sasa mpaka hapo itakapo tangazwa tena.
“Kwa mamlaka niliyopewa na sheria ya mifugo natangaza kuanzia sasa wilaya ya Ludewa itakuwa chini ya karantini kutokana na ugonjwa huu wa homa ya nguruwe mpaka hapo tutakapo tangaza tena kuendelea na shughuli hizo”.
Aidha ameongeza kuwa kwa yeyote atakaye bainika kuendeleza huduma hizi atachukuliwa hatua kali za sheria ambapo moja ya sheria hizo ni kifungo cha miezi sita jela, faini ya shilingi milioni 1,200,000 ama vyote kwa pamoja.
Pia amewaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuutokomeza ugonjwa kwa haraka
“Naomba tutoe ushirikiano kwenye kuhakikisha hakuna mtu anavunja mashariti yaliyowekwa, kwani tukifanya hivyo huu ugonjwa huwa unaisha haraka sana (unapita) na baada ya hapo tunaendelea na utaratibu wetu wa kuchinja au kula kitimoto kama kawaida.” Amesema Mkomba