Mauaji yalivyotikisa mwezi Januari

Wakati wengi wakisema mwezi Januari ni mwezi wa majanga, wengi wao humaanisha kuwa ni mwezi mgumu katika suala la kiuchumi, kwani familia nyingi zinakuwa zinayumba katika kipindi hiki kutokana na kwamba mwezi huu unakuwa na matumizi mengi sana  ya pesa ikiwemo kulipia ada za shule pamoja na kulipia kodi ya nyumba.

Hata hivyo fikra hizi katika mwezi huu zimeonekana kufunikwa na matendo ya kikatili yaliyotikisa ndani ya mwezi huu Januari huku raia wakibaki midomo wazi kwamba nini kinaendelea.

Tangu kuingia January 2022, kumekuwa na matukio mengi ya mauaji na mtukio hayo yamehusisha, imani za kishirikina, wivu wa mapenzi na tamaa ya umiliki mali.

Mnamo January 18, Waziri wa Mambo Ndani Hamad Masauni alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari 1 hadi 15 mwaka huu matukio 22 ya mauaji yanayohusisha ndugu wa familia moja na wivu wa kimapenzi yameripotiwa.

Wakati Waziri Masauni akisema hayo matukio mapya ya mauaji yakaendelea kutokea na kwa sasa unaweza kusema ni Kiza Kinene kimetanda juu ya mauaji hayo.

Kufuatia mauaji hayo Wanaharakati, Viongozi wa dini na Viongozi wa Serikali wamekuwa wakiyalaani na ni hivi karibuni tu Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, alimuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi-IGP Simon Sirro, kulivalia njuga haraka iwezekanavyo kuhakikisha kwamba wanakomesha mauaji hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema mwezi huu wa Januari, kumeripotiwa matukio mbalimbali ya mauaji ya kikatili, ambayo yameleta huzuni na kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu. 

Amesema LHRC imekusanya takribani matukio 20 ya mauaji hayo, yaliyoripotiwa katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Njombe, Katavi, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Dar es Salaam, na Mara.

Ameyataja baadhi ya matukio hayo ni la Mkoa wa Mtwara, ambapo Januari 23, mwaka huu kuliripotiwa tukio la askari polisi saba ambao walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumuua Mussa Hamisi (25), mkazi wa Kijiji cha Ruponda wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi. 

Sababu za kuuawa kwa Mussa ziliziripotiwa kuwa ni kitendo chake cha kudai fedha zake kiasi cha shilingi milioni 33.7 ambazo polisi hao walidaiwa kuzichukua baada ya kumpekua na kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, ACP Marck Njera mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022.

Mauaji haya ni mfano wa mauaji yanayofanywa na maafisa wa vyombo vya dola na kitendo hiki ni ukiukwaji wa haki ya kuishi. Kitendo cha kuchukua na kukataa kurejesha fedha za Mussa pia ni ukiukwaji wa haki ya kumiliki mali,” amesema Henga.

Pia tukio lingine amelitaja ni lile lilitokea mkoani Mwanza, ambapo wanawake watatu waliuwawa na miili yao kutupwa katika eneo la Mecco Kusini wilayani Ilemela.

LHRC inalaani kitendo hiki cha ukatili dhidi ya wanawake na tunatoa rai kwa jeshi la polisi kufanya uchunguzi na kuhakikisha watu waliofanya vitendo hivi ya ukatili wanafikishwa mahakamani,” amesema Henga.

https://mwanzotv.com/2022/01/27/amuua-mjamzito-kisa-deni-la-gunia-mbili-za-mahindi/
https://mwanzotv.com/2022/01/26/ashiriki-kumuua-mama-mkwe-wake-kwa-tuhuma-za-ushirikina/

Kwa sasa waweza sema ni kama kuna roho ya kishetani inayowazunguka watuhumiwa, kwani wengi wao hufanya mauaji hayo na kisha wao wenyewe hujaribu kujinyonga ili kupoteza ushahidi