Bei ya mafuta imepanda tena mwezi huu na kuivuka ile ya Julai licha ya Serikali kuendelea kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwa mwezi Agosti.
Julai mwaka huu bei ya rejareja jijini Dar es Salaam ilikuwa shilingi 3,220 kwa lita moja ya petroli na shilingi 3,143 kwa dizeli huku mafuta ya taa yakifika shilingi 3,442.
Aidha, katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne Agosti 2, 2022 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), bei ya rejareja jijini Dar es Salaam baada serikali kuweka ruzuku ya shilingi bilioni 100, itakuwa shilingi 3,410 kwa lita moja ya petroli na shilingi 3,322 kwa dizeli huku mafuta ya taa yakifika shilingi 3,765.
Katika mkoa wa Tanga itakuwa shilingi 3435 kwa lita moja ya petrol na shilingi 3,349 kwa lita moja ya dizeli. Mkoa wa Mtwara itakuwa shilingi 3,393 kwa lita moja ya petrol ilihali dizeli itakuwa shilingi 3,351.
Maumivu yatakuwa makali zaidi mkoani Kagera hasa katika Wilaya ya Bukoba ambako lita moja ya petroli itauzwa shilingi 3,625 na dizeli shilingi 3,950 na mafuta ya taa ni shilingi 3,981.
Ewura imesema bei hizo mpya ambazo zitaanza kutumika leo Jumatano zimejumuisha ruzuku ya shilingibilioni 100 iliyotolewa na Serikali.
Kama ruzuku hiyo isingetolewa, lita ya petrol ingeuzwa shilingi 3,630, dizeli shilingi 3,734 na mafuta ya taa shilingi 3,765 jijini Dar es Salaam wakati Bukoba ingekuwa shilingi 3,845 kwa petroli na shilingi 3,950 kwa dizeli. Mafuta ya taa hayana ruzuku.
“Bei ya mafuta katika soko la dunia imeendelea kupanda na bei ya mafuta katika soko la ndani kupanda vilevile. Lakini katika kupunguza kupanda kwa bei hizo, serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kupunguza makali ya bei hizo,” imesema taarifa hiyo.