Serikali imesema magari yataanza kulipia fedha yanapopita kwenye Daraja la Tanzanite na katika barabara nyingine mbili za haraka ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro (Expressway) na ile ya Igawa – Songwe -Tunduma (Expressway) kwa kuwa zote zina sifa za kutozwa fedha.
Katika hotuba ya Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa siku chache zilizopita bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alisema serikali inaendelea kuboresha sekta ya uchukuzi nchini kwa kuendeleza utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara ili kufungua fursa za kiuchumi.
Alisema katika kutekeleza miradi hiyo ya ujenzi wa barabara kama sehemu ya kufungua fursa na kuiunganisha nchi na mataifa jirani, serikali itamalizia ujenzi wa barabara zinazounganisha mikoa na kwamba wakandarasi wapo kazini. Alisema katika ujenzi huo, Daraja la Tanzanite lililopo maeneo ya Salender Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 1.03 lililojengwa baharini jirani na ufukwe wa Coco litawekewa malipo ya fedha kwa sababu lina sifa za kufanya hivyo.
Daraja hilo lina njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu, limejengwa pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2 na linaunganisha Hospitali ya Aga Khan na barabara za Obama, Kenyatta na Toures mkoani humo na kubadilisha mandhari yake.
Dk Mwigulu alitaja barabara nyingine zitakazowekwa tozo ya barabara kwa sababu zina sifa za kufanywa hivyo ni ile ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro ambayo ujenzi wake ukikamilika utakuwa na urefu wa kilometa 158 na Barabara ya Igawa – Songwe -Tunduma ambayo ikikamilika ujenzi wake itakuwa na urefu wa kilometa 218. Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja akizungumzia hilo alisema serikali inapowasilisha bajeti kuu ina maana kila kinachowasilishwa kiko kwenye mpango wa kutekelezwa katika mwaka wa fedha unaohusika.
“Bajeti na mambo yanayosomwa kwenye bajeti kuu yakiwasilishwa bungeni ina maana yako kwenye mpango wa utekelezaji kwa bajeti husika na hiyo hufanyika baada ya bunge kuridhia,” alisema Mwaipaja. Hivi karibuni Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ilisema inatarajia kuanza kufanya kazi ya usanifu wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka KibahaChalinze-Morogoro.
Ofisa Mwandamizi wa Jamii kutoka Tanroads, Gibson Mwaya alibainisha hayo katika taarifa yake mbele ya kikao maalumu kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge. Mwaya alisema kazi hiyo ilitarajiwa kuanza siku chache baadaye na itafanywa kwa miezi miwili na baadaye ripoti ya awali itakabidhiwa kwa Mtendaji Mkuu na baada ya hapo kazi ya usanifu huo ripoti hiyo itaeleza namna ambavyo kazi inapaswa kufanyika pamoja na gharama halisi za ujenzi wa barabara hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge akizungumza katika kikao hicho alisema barabara hiyo itajengwa njia mbili kwenda na njia mbili kurudi mpaka kufika mkoani Morogoro ikiwa sawa na kilomita 158 na kusema njia hizo zinaitwa njia za haraka. “Kazi hiyo itakuwa na athari chanya katika nchi yetu, nchi za SADC na hata Afrika Mashariki,” alisema Kunenge.