Mauzo ya nyama nje ya nchi yaongezeka

Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Tanzania (TMB), Dk Daniel Mushi amesema mauzo ya nyama nje ya nchi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 15 mwaka jana yalifikia tani 5,158.93, sawa na ongezeko la asilimia 21.7 ikilinganishwa na tani 4,239.42 zilizouzwa kipindi kama hicho mwaka 2021 huku nchi ya Qatar ikiongoza kwa kununua tani 504.

Amesema katika kipindi cha Novemba mwaka jana, Tanzania iliuza nje ya nchi tani za nyama 1,423 zenye thamani ya dola za Marekani 5,370,187.70 sawa na zaidi ya Sh bilioni 10 za Kitanzania.

Kwa mujibu wa Dk Mushi, ni kwamba  kiasi hicho kilichouzwa ni sawa na ongezeko la asilimia 125, ikilinganishwa na tani 632 zilizouzwa Oktoba 2022.

“Tani 1,423 za nyama zilizouzwa Novemba mwaka 2022, ni sawa na ongezeko la asilimia 62 ikilinganishwa na tani 878 zilizouzwa Novemba mwaka  2021, mpaka hapo zimeongezeka tani 545,” alisema Dk Mushi.

Mchanganuo wa tani hizo 1,423 za nyama zilizouzwa ni ya mbuzi tani 1,047, kondoo tani 343, ng’ombe tani 32, kuku tani 0.67 na nyama ya nguruwe tani 0.2.

Meneja wa Idara ya Masoko TMB, John Chassama alisema zaidi ya nchi sita zimeshiriki kununua tani hizo ikiwamo Qatar iliyonunua tani 504, Oman (334), UAE (267), Saudi Arabia (125), Kuwait (56), Bahrain (50) na China tani 38.

Katika hatua nyingine, Chassama alieleza sababu za nyama ya mbuzi kuuzwa zaidi kuliko nyingine ni kutokana na mahitaji yake kuwa juu zaidi sokoni na upatikanaji wa mbuzi kama malighafi kwenye viwanda vya nyama ni rahisi ikilinganishwa na mifugo mingine.

Alisema kwa namna kiwango cha nyama kinachouzwa nje inavyoendelea kukua, ndivyo mahitaji ya mifugo ambayo ni malighafi kwenye viwanda vya nyama inaongezeka.