Mbowe afanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle.

Mbowe amekutana na Balozi Battle ikiwa zimebaki siku 6 kuelekea maandamano ya amani yanayotarajiwa kufanyika Januari 24,2024.

Wawili hao wamejadili masuala ya mabadiliko ya kidemokrasia nchini Tanzania, kwa mujibu wa Balozi Battle aliyeandika ujumbe wake katika ukurasa wake wa X

Nikinukuu ujumbe huo umesema “Nimefurahi kuungana tena na Freeman Mbowe kujadili maendeleo ya mabadiliko ya kidemokrasia nchini Tanzania,” ameandika Balozi Battle kupitia mtandao huo wa kijamii

Hii si mara ya kwanza kwa wawili hao kukutana, itakumbukwa kwamba Novemba 3, 2023 walikutana ambapo Mbowe katika ukurasa wake wa X aliandika akieleza kwamba miongoni mwa mengi waliyojadili, ni changamoto kadhaa zinazokabili ujenzi wa demokrasia nchini Tanzania.

Pia, alimshauri kuhusu umuhimu wa kuendeleza juhudi shirikishi zitakazowezesha ujenzi wa demokrasia imara itakayoweka misingi ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii nchini Tanzania.

Aidha, amemueleza Balozi hofu yake kuhusu uharibifu wa mazingira katika Mlima Kilimanjaro na mfumo wake wa ikolojia.

Itakumbukwa Januari 13 mwaka huu Freeman Mbowe aliutangazia umma wa Watanzania kuwa kutafanyika maandamano ya amani ambayo yana lengo la kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa uchaguzi nchini.kuhusu miswada ya sheria iliyowasilishwa hivi karibuni.

Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Kwa mujibu wa CHADEMA maandamano hayo yatafanyika kwa njia mbili, yaani kutoka Mbezi Mwisho na kutoka Buguruni lakini waandamanaji wote katika maeneo hayo watahitimisha maandamano yao Ofisi za Umoja wa Mataifa.

Mkutano wa Leo wa  kati ya Mbowe na Balozi wa Marekani umeonekana kuleta maswali kwamba kwanini CHADEMA wanatumia washirika wakubwa katika kuelekea maandamano?