Mbowe kuongoza kongamano la DUA Afrika Kusini

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe leo ataondoka  nchini Tanzania kwenda Afrika ya Kusini kwa ziara ya kikazi ya siku saba.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema imeeleza kuwa akiwa Afrika ya Kusini, Mbowe kama Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA) ataongoza kongamano la kwanza la umoja huo litakalodumu kwa siku nne.

Kongamano hilo litahudhuriwa na vyama wananchama wa DUA, viongozi  wa serikali, mabalozi  na wabunge wanaotokana na vyama wanachama wa DUA pamoja na mashirika na taasisi mbalimbali za kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo akisaidiana na Waziri Mkuu Mstaafu wa Canada, Stephen Harper anatarajiwa kuwa mgeni wa heshima wa kongamani litakaloangazia masuala ya uchumi, ulinzi na usalama, demokariasia pamoja na biashara barani Afrika.

Mbowe anatarajiwa kuhitimisha ziara yake Afrika ya Kusini kwa kuongoza kikao cha Bodi ya uongozi ya DUA kitakachofanyika Aprili 30, 2023 kama kilele cha kongamano hili ambalo litahudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika atakayeongoza ujumbe wa chama nchini Afrika ya Kusini.

Mrema amesema, Mbowe akiwa Afrika Kusini atakutana na wafanyabiashara mbalimbali barani Afrika Mei Mosi, 2023 kwa lengo la kujadiliana mikakati mbalimbali ya kisera itakayochochea uondoshwaji wa vikwazo vya ufanyaji wa biashara Afrika ikiwa ni sehemu ya kuwezesha utumiaji wa fursa zitokanazo na eneo huru la kibishara la Afrika “The African Continental Free Trade Area” (AfCFTA).