Search
Close this search box.
East Africa

Kesho Machi 4 ndio siku iliyopangwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na  Uhujumu Uchumi kuanza kusikiliza utetezi wa washtakiwa wa kesi ya Ugaidi inayomuhusisha mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Mahakama hiyo Februari 18,2022 iliwakuta na kesi ya kujibu Mbowe na wenzake katika kesi ya ugaidi inayowakabili, hatua ambayo ilikuja baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake kwa kuwaita mahakamani mashahidi 13 kati ya 24 iliokuwa imepanga kuwaita, huku ikitoa vielelezo 39.

Hata hivyo baada ya uamuzi huo wa mahakama, jopo la Mawakili wa utetezi waliimbia mahakama hiyo kuwa wateja wao watajitetea chini ya kiapo ambapo kila wakili aliiambia mahakama juu ya mashahidi watakaokuja kutoa ushahidi wa utetezi kwa washtakiwa hao.

Wakili anayemuwakilisha mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ambaye ni Wakili Jeremiah Mtobesya aliiambia Mahakama hiyo kuwa mteja wake atajitetea mwenyewe lakini pia anatarajia kuita mashahidi wengine watano, hivyo yeye atakuwa ni wa sita.Pia ameeleza katika kuleta utetezi atatoa vielelezo vitano.

Wakili John Mallya anaye muwakilisha mshtakiwa wa pili, siku hiyo aliiambia mahakama kuwa mteja wake ataleta ushahidi wake chini ya kiapo na mashahidi wawili pamoja na vielelezo vinne.

Kwa upande wake Wakili Fredrick Kiwelu  anayemuwakilisha mshtakiwa wa tatu, aliiambia Mahakama kuwa mteja wake atajitetea chini ya kiapo, na atakuwa na mashahidi watano pamoja na vielelezo vitano:

Aidha Wakili Peter Kibatala anayemuwakilisha mshtakiwa wa nne, ambaye ni Mbowe alisema mteja wake atajitetea kwa kiapo, ataleta mashshidi 10 na yeye wa 11 na ataleta vielelezo 20.

Mbowe na wenzake hivi sasa wanakabiliwa na mashtaka 5 baada ya shtaka moja kufutwa kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuleta uthibitisho.

Mbali na Mbowe wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Comments are closed