Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema moto wa siasa umewashwa ndani ya chama hicho, huku akiahidi kufanya kazi usiku na mchana kuwafikia watanzania.
Mbowe alitoa kauli hiyo April 10,2022 wakati wa ziara yake katika jimbo la Kawe jijini Dar es salaam, ikiwa ni kampeni ya mguu kwa mguu kuzungumza ana kwa ana na wananchi pamoja na kukusanya fedha za kujenga chama.
Alisema ziara hiyo ni mwendelezo wa oparesheni ya ‘join the chain’ yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa chama hicho pamoja na kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Tegeta na kata ya Kunduchi, Mbowe alisema matembezi hayo yatakuwa ni kwa miguu ndani ya mitaa ya jiji hilo, na kwamba pamoja na mambo mengine ni kuwashukuru Watanzania kwa kupigania uhuru wake alipokuwa gerezani.
“Na ninatembea kama mnavyoniona kuwasalimia wananchi, nikitambua namna mamilioni ya Watanzania walivyolilia uhuru wangu na vijana wangu nilipokuwa gerezani. Kwa hiyo napita kuwasalimia kuwashukuru namna ambavyo mlitetea haki yetu na uhuru wetu, asanteni sana na Mungu awabariki,” alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa kazi ya siasa haijafika mwisho bali imechochewa moto kwa kuwa chama hicho kitatembea usiku na mchana kuhakikisha kuwa wanaliamsha taifa ili litambue namna ya kutetea watu wake.
“Tutatembea usiku na mchana, kwa jasho na damu, kuhakikisha tunaliamsha taifa hili, lijitambue ,lijue namna ya kutetea haki na uhuru wa nchi yake, namna ya kuibana serikali yetu itambue kwamba maisha ya wananchi yamekuwa magumu, waache kuongeza tozo, ili maisha ya wananchi yawe nafuu,” alisema
Aidha amesema wajibu wa kulitetea taifa ni wa kisiasa na kuwataka wananchi wa Tegeta kumuunga mkono katika wajibu huo ili kupaza sauti kwa pamoja.
“Lazima tupaze sauti yetu, hatuwezi kuendelea kuwa taifa la kuoneana, kudhulumiana, la kunyanyasana na taifa la ubaguzi wa kiitikadi. Asanteni Kawe kwa mapokezi mazuri, Tegeta nitaendelea kuwa na ninyi,hakuna kulala mpaka kimeeleweka,” alisema Mbowe
Baada ya kuzungumza Mbowe alianza kukusanya michango ya hiyari kutoka kwa wananchi hao kwa ajili ya kusaidia kujenga chama huku akisisitiza kuwa kitajengwa na wananchi wenye uwezo mdogo ambao hutoa fedha zao kama sadaka ya ukombozi na siyo matajiri pekee.