Search
Close this search box.
Africa
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amedai kuwa kauli ya Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson, iliyodai kuwa Halima Mdee na wenzake 18 wako bungeni kihalali, kwa kuwa CHADEMA  hawajawasiisha barua ya kuwafukuza, “ni ulagai wa kisiasa na kuwafanya mazuzu

Mbowe ameyasema hayo leo, wakati akitangaza maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho, iliyoketi Machi 16 hadi usiku wa kuamkia Machi 17,2022.

Mbowe alikuwa akijibu swali na wanahabari kutaka kujua kauli ya chama chake kufuatia hatua ya Spika Tulia kukiri kuwatambua wabunge hao 19 wakiongozwa na Halima Mdee ni wabunge halali wa Chadema.

“Hatuwezi kila siku kuzungumzia wabunge 19, kauli za Spika ni ulaghai wa kisiasa, anajua Spika kwamba wale wabunge hawakutokana na chama chetu na wameshafukuzwa. Ule ni kutufanya sisi mazuzu. Wameshaandikiwa barua na chama kuwa wamefukuzwa,” amesema Mbowe.

Amesema, kitendo cha wabunge hao 19 kuendelea kubaki Chadema, kinaleta mpasuko kwa Taifa.

“Issue sio kukubali wabunge 19, tunapowakataa wabunge 19 tunakataa ukiukwaji wa sheria za nchi. Forgery (kughushi) iliyofanyiwa Taifa na kwenda kubariki ubatili wa aina hiyo, hatutakubali kutokea,” amesema Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe amesema rufaa za wabunge hao zitasikilizwa ama kutolewa maamuzi katika kikao cha Baraza Kuu la Chadema, ambacho kinatarajiwa kufanyika Aprili 25,2022.

Mbali na Mdee na wengine waliofukuzwa Chadema kwa madai ya usaliti ni, Nusrat Hanje, Grace Tendega. Hawa Mwaifunga, na Jesca Kishoa.

Wengine ni, Agnesta Lambat. Tunza Malapo. Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Wabunge hao walivuliwa uanachama wa Chadema mnamo Novemba 17,2020, siku tatu baada ya kuapishwa na aliyekuwa Spika wa Bunge,  Job Ndugai, kuwa wabunge viti maalumu kupitia chama hicho.

Mdee na wenzake walituhumiwa kwa makosa ya kusaliti msimamo wa Chadema wa kutopeleka wabunge wa viti maalum bungeni, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kwa madai kwamba mchakato wake haukuwa huru na wa haki.

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zilikanusha madai hayo zikisema kwamba ziliendesha mchakato huo katika misingi ya ukweli, haki na uwazi.

Comments are closed