Mbunge wa Ngorongoro ashangazwa Polisi kumkamata bila kibali cha Spika

Mbunge wa Ngorongoro Emmanuel Ole Shangai (CCM),ameshangazwa na hatua ya polisi kumkamata bila kibali cha Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kama ambavyo taratibu za ukamatwaji zinapaswa kufanywa kwa wabunge kutokana na kinga ya bunge waliyonayo.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo usiku wa kuamkia leo muda mfupi baada ya kuachiliwa huru kutokana na kushikiliwa na polisi tangu tarehe 21 Agosti 2023. 

Mbunge huyo alidaiwa kushikiliwa na jeshi hilo, akiwa njiani kuelekea kituo cha Polisi wilayani Karatu, kutokana na tuhuma za kuhusishwa kupanga tukio la kushambuliwa waandishi wa habari huko.

“Ninachoshangaa wote wanajua, polisi ndio wanasimamia sheria zetu na Bunge ndio linatunga sheria niliamini kwamba kama walikuwa wananihitaji na hicho ndio nilikuwa nasubiri wangemuandikia Spika barua alafu Spika anijulishe.

“Nakumbuka mwaka jana Aprili niliitwa kuhojiwa kuhusiana na suala la Loliondo, Spika ndio alitoa kibali cha mimi kuhojiwa nashangaa leo kwanini hawakusubiri mpaka Spika atoe barua… najua kuna presha za kisiasa na mimi ni mwanasiasa nitaendelea kuishi kwenye siasa,” amesema.

Akizungumza baada ya kuachiwa Ole Shangai amesema kwa siku tatu tangu alipokamatwa aligoma kula na baada ya kujisalimisha Karatu alisafirishwa saa saba usiku Agosti 22 kurudishwa Arusha na alikuwa Kituo cha Diplomasia jijini Arusha.

“Pia nimejifunza kuwa binadamu unaweza kukaa siku tatu bila kula na hautakufa na hata ningekaa siku saba nisingekula siku saba,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amewataka wananchi wajue yeye ni kiongozi wao hata akikamatwa mara 10 ataendelea kuwa na msimamo wao kwa sababu walimchagua kwa ajili yao na kwa kuwa yupo upande wa wananchi lazima apate matatizo, na hilo halitomrudisha nyuma hata siku moja.