Mchango wa kununua gari jipya la Lissu wafikia milioni 24.9 

Mchango wa fedha za kumnunulia gari Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu umefikia Sh. milioni 24.9 ndani ya siku saba tangu kuanzishwa kwa harambee hiyo.

Kupitia ukurasa wa X Lissu alithibitisha kupokea kiasi hicho cha fedha na kuomba wadau waendelee kumchangia apate gari hilo “kwa ajili ya harakati za ukombozi”.

Itakumbukwa kuwa Mei 17 mwaka huu, wafuasi wa mwanasiasa huyo wakiongozwa na Mwanaharaki Maria Sarungi, waliazimia kumchangia fedha mwanasiasa huyo anunue gari jipya ili lile la zamani ambalo lilishambuliwa kwa risasi lihifadhiwe kwa ajili ya ukumbusho.

“Tumekamilisha wiki moja ya mchango. Hadi sasa tumepokea Sh. 24,956,282.00 kutoka kwa wachangiaji 2,243. Kwa wastani, kila siku wachangiaji 320 wametoa Sh. 11,126.30 kila mmoja,” aliandika Lissu kwenye ukurasa wake wa X.

Mei 17 Lissu alikabidhiwa gari lake aina ya Toyota Land Cruizer V8, VXR na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, ikiwa iimepita takriban miaka saba tangu aliposhambuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Area D, jijini Dodoma Septemba 7, 2017.

Baada ya kukabidhiwa gari hilo, Lissu alieleza lengo lake la kulitengeneza gari hilo ili kulitumia kwenye shughuli za kisiasa, jambo ambalo lilipingwa na wafuasi wake wakisisitiza watamnunulia gari jipya. Hilo liwekwe Makumbusho ya Taifa ili vizazi vijavyo vione yaliyotokea.

Ndani ya saa 48 tangu Maria kuweka namba za malipo kwa ajili ya kukusanya fedha hizo kupitia mitandao ya kijamii ya X na Instagram zilikusanywa Sh. milioni 15.

Lengo la mchango huo ni kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kinapatikana kiasi cha fedha kitakachotosheleza kununua gari linalofanana na lililoshambuliwa kwa risasi ili Lissu aendelee na shughuli zake za kisiasa.

Katika ukurasa wake wa X, Maria juzi aliendelea kuhamasisha wafuasi na wapenzi wa kiongozi huyo kuchanga ili kiasi hicho cha fedha kipatikane na gari linunuliwe kwa muda waliopanga.

“Tukishikamana tunaweza, kuhamasishana kila mtu unayemjua atoe Sh. 1,000 au 500, tukiamua watu 10,000 kutoa Sh. 1,000 kwa siku tunapata milioni 10 ndani ya mwezi tunamalizia kilichobaki,” aliandika Maria kwenye ukurasa wake wa X.