Mwanaharakati na kada wa CHADEMA Mdude Nyagali ameijibu barua ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Mbeya, iliyomtaka kukabidhi simu zake na vifaa vingine vya kielektroniki kwa ajili ya kufanyia uchunguzi kuhusiana na kauli na machapisho aliyoyatoa mnamo tarehe 9 Julai,2023.
Kufuatia hayo katika barua hiyo aliyoijibu Mdude kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Mbeya, ameeleza kwamba tarehe 14 Julai alivyokamatwa na kuwekwa kizuizini kinyume na sheria bila kumueleza tuhuma zinazomkabili na kumnyima dhamana huku akijua kuwa ni kinyume na sheria na kumtaka aandike maelezo yake manmo Julai 16 saa nane mchana jambo ambalo alikataa na kutaka kutoa maelezo yake Mahakamani.
Aidha ameeleza kuwa mnamo tarehe 17 majira ya usiku wa saa nne na nusu, akiwa kuzuizini kinyume na sheria aliruhusiwa kutolewa lakini katika hali ya kushangaza na kustaajabisha akiwa anatolewa mahabusu alikabidhiwa barua inayomtaka kukabidhi vifaa vyake vyote kwa ajili ya uchunguzi bila kubainsha kinachotakiwa kuchunguzwa.
Pamoja na hayo Mdude katika barua hiyo pia ameeleza wasiwasi wake juu ya mwenendo mzima wa kumtaka kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya uchunguzi kutokana na madai kwamba Mkuu huyo wa upelelezi amemtaja kama aliyehusika kumuwekea madawa ya kulevya nyumbani kwake mnamo mwaka 2020 wakati alipokwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake kwenye kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili wakati huo
Hivyo kufuatia maelezo ya kwenye barua hiyo aliyoichapisha Mdude hii leo, amemtaka Mkuu huyo wa Upelelezi kwamba kama kuna kifaa chochote cha kielektroniki kinachotakiwa kwa ajili ya uchunguzi basi kidaiwe kwa njia ya Mahakama na ombi hilo liweke wazi maeneo yanayotakiwa kufanyiwa uchunguzi.
Mdude ameweka wazi kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano wowote unaohitajika katika kukamilisha uchunguzi unaotakiwa.
Itakumbukwa Mdude alishikiliwa na Polisi siku ya Ijumaa na kwa mujibu wa wakili wake ni kwamba amefunguliwa jalada la kutangaza taarifa za uchochezi na chuki dhidi ya Serikali kupitia simu yake ya mkononi huku wakieleza endapo atakubali kuikabidhi Polisi itakuwa kielelezo cha ushahidi na kumfikisha Mahakamani.