Meli kubwa iliyobeba watalii 2,210 yatua Bandari ya Dar

Meli kubwa iliyobeba watalii 2,210 kutoka Canada, imewasili alfajiri ya leo Jumanne Januari 16, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Meli hiyo inayoitwa Norwegian Cruise Line Dawn yenye urefu wa mita 294, imetajwa kuwa kubwa zaidi kuwasili katika bandari zote nchini tangu kuanzishwa kwake. Norwegian Cruise Line Dawn ilianza kufanya kazi mwaka 2002 ikiwa na thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni.

Norwegian Cruise Line Dawn pia ina kimo cha mita 59, ikienda kwa kasi ya kilomita 46 kwa saa na ina wafanyakazi zaidi ya 1,000.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho ameeleza kwamba  hadi inafika Tanzania, meli hiyo imepitia katika bandari tofauti ikiwemo ile ya Mombasa, nchini Kenya na ina uwezo wa kubeba abiria 4,700, japo waliowasili ni watalii 2,210 pamoja na wafanyakazi zaidi ya 1,000.

“Tuna furaha kuona kampeni ya Royal Tour inaendelea kuzaa matunda, hawa watalii walioshuka wanakwenda katika vivutio mbalimbali ikiwemo hifadhi ya Selous,” amesema na kuongeza kuwa;

“Ujio wa meli hii umetokana na usalama pamoja na maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwemo kuongeza kina na lango kuu lililowezesha kupitisha meli hii, matarajio yetu ni kuhudumia meli zenye urefu wa mita 305 kwa siku za usoni,” amesema Mrisho.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, meli hiyo inatarajiwa kuondoka jioni ya leo kuelekea Msumbiji.

Mara ya mwisho kwa meli ya kitalii kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, ilikuwa Novemba 10, 2022; ambapo meli ya Zaandam inayomilikiwa na Kampuni ya Holland American Line ilitia nanga kwa siku mbili kabla ya kuelekea Zanzibar, ikiwa na watalii 1,500.

Aprili 8, 2022 Bandari ya Dar es Salaam ilipokea meli kubwa aina ya Frontier Ace iliyobeba magari 4,041 ikiwa ni ya kwanza kubeba mzigo mkubwa wa magari tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Nahodha Mkuu wa TPA, Abdullah Mwingamno amesema kabla ya kuja meli hiyo wiki tatu zilizopita, alikuwa nchini Ujerumani kwenye mazoezi ya kuingiza meli kubwa kwenye lango la Bandari ya Dar es Salaam na walifanikisha kuingiza meli yenye urefu wa mpaka mita 350.

“Licha ya kuwa wataalamu waliofanya maboresho walisema uwezo wa gati zetu ni kuingiza mweli yenye urefu wa mpaka mita 305, lakini tunaweza kufanya zaidi ya hivyo na hili limethibitisha, tunaamini sasa tutavutia meli nyingi zaidi,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTP), Damas Mfugale amesema watalii waliokuja na meli hiyo watatembelea mji wa kihistoria ya Bagamoyo, wengine watakwenda Hifadhi ya Selous kwa ajili ya kutazama wanyama na wengine watafanya utalii katika jiji la Dar es Salaam.