Mfalme Zumaridi amkataa hakimu

Mawakili wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili, Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wafuasi wake nane wameonesha kutokuwa na imani na Hakimu anayeendesha kesi hiyo na kuiomba Mahakama kutolea maamuzi ya sababu walizowakilisha ili ushahidi uendelee kutolewa.

Ombi la kumkataa hakimu anayesikiliza kesi yake, Monica Ndyekobora wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, limewasilishwa leo Julai 11, 2022 na Steven Kitale, wakili wa Mfalme Zumaridi wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi.

Katika kesi hiyo Mfalme Zumaridi na wenzake nane wanakabiliwa na shtaka la kushambulia na kumsababishia majeraha Ofisa wa Jeshi la Polisi na kumzuia Ofisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yake.

Bila kuweka wazi sababu za mteja wake kutokuwa na imani na hakimu, Kitale amesema upande huo wa utetezi unasubiri maamuzi ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Monica Ndyekobora kuhusu hoja zilizowasilishwa na mshtakiwa mezani kwake.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga ameiambia mahakama kwamba kesi hiyo imeitwa leo kwa ajili ya kusikiliza ushahidi huku upande huo ukiwa umeleta mashahidi wawili kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Luvinga ambaye aliambatana na wakili, Deogratius Lumanyika amewataja mashahidi hao kuwa ni Askari wa Jeshi la Polisi, WP4592 Sajenti Paulina na F1468 Sajenti Joanes Mlashani.

Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobora ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 18,2022 itakapoitwa kwa ajili ya kutoa uamuzi wa hoja zilizowasilishwa na wakili wa Zumaridi mbele ya mawakili wa Jamhuri na utetezi walipokutana ofisini kwake.