Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania (NBS) imesema mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia Februari, mwaka huu umepungua hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 4.0 ulivyokuwa mwaka unaoishia Januari.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu za Kijamii, Ruth Minja, alisema mfumuko wa bei kwa taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
Minja alisema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwaka unaoishia Februari kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi hicho ikilinganishwa na Januari.
“Bidhaa za vyakula zilizoonyesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, ikilinganishwa na mwaka ulioishia Januari ni pamoja na: matunda (kutoka asilimia 9.5 hadi asilimia 5.2); mbogamboga (kutoka asilimia 5.0 hadi asilimia 3.7); kunde (kutoka asilimia 7.1 hadi asilimia 2.6).
“Njegere (kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 4.2); siagi (kutoka asilimia 6.6 hadi asilimia 6.5); tambi (kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 3.9) na bidhaa za ngano za kutoka (kutoka asilimia 8.4 hadi asilimia 5.8).”
Alisema baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilizoonyesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari ikilinganishwa na ule wa Januari ni pamoja na: nguo za watoto (kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 2.9) na mkaa (kutoka asilimia 6.4 hadi asilimia 6.1).
Nyingine ni magodoro (kutoka asilimia 7.3 hadi asilimia 6.2) na huduma za vyakula kwenye migahawa kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 1.9.
“Kwa ujumla mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Febuari umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.3 kwa mwaka ulioishia Januari mwaka huu,” alisema.
Aidha mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari nao umepungua kwa asilimia 2.7 kutoka asilimia 3.1 ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari.
Alisema Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari umeongezeka hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 2.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari na Kenya umepungua hadi asilimia 5.08 kutoka asilimia 5.39.