Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi imewahukumu kutumikia miaka 30 jela, Majid Khalid almaruufu Alsalimi (36) mkazi wa Mtaa wa Madukani, na Wahab Amory (29) mkazi wa Mtaa wa Kawajense, Manispaa ya Mpanda; baada ya kupatikana na kosa la kulawiti.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 9,2023 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi, Gway Sumaye, ambapo mbali na adhabu hiyo, wawili hao wanatakiwa kumlipa muathirika wa tukio hilo shilingi milioni mbili kila mmoja ikiwa ni fidia.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, watu hao walitenda kosa hilo la kumlawiti mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa) kwa nyakati tofauti, jambo ambalo ni kinyume na kifungu namba 154(1) (a) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
Watu hao wanadaiwa kutenda kosa hilo maeneo ya madukani, Shanwe na Kawajense Manispaa ya Mpanda kwa nyakati tofauti kuanzia March 1, 2022 hadi March 2023.
Taarifa za kimahakama zinaonyesha kuwa kesi ilifunguliwa na kuanza kusikilizwa mahakamani hapo April 24, 2023.