Miaka 31 ya uhuru wa Ukraine iliyojaa misukosuko ya vita

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kwamba nchi yake itapambana na uvamizi wa Urusi “hadi mwisho” na haitafanya “makubaliano yoyote au maelewano”.

Ameyasema hayo leo ikiwa ni siku ya miaka 31 ya uhuru kutoka kwa Muungano wa Kisovieti

Ukraine inaadhimisha uhuru wake ikiwa katika hali ngumu ya misukosuko ya vita vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa hilo ambalo sasa watu wake wanaishi kwa hofu juu ya muafaka wa maisha yao

“Hatujali una jeshi gani, tunajali ardhi yetu tu. Tutaipigania hadi mwisho,” Zelensky alisema katika hotuba yake ya video leo Jumatano, ambayo pia inaadhimisha miezi sita tangu uvamizi huo uanze.

“Tumeshikilia kwa nguvu kwa miezi sita. Ni ngumu lakini tumekunja ngumi na tunapigania hatima yetu,” alisema.

“Kila siku mpya ni sababu ya kutokata tamaa. Baada ya safari ndefu namna hii hatuna haki ya kutoendelea hadi mwisho,” alisema.

Akizungumzia Urusi, aliongeza: “Hatutajaribu kupata maelewano na magaidi.

“Kwetu sisi Ukraine ni Ukraine nzima. Mikoa yote 25, bila makubaliano yoyote au maelewano.”

Maadhimisho ya kumbukumbu ya uhuru au la, milipuko ya mabomu bado inatishia Ukraine na hasa mji mkuu wa Kyiv. Wasiwasi umetanda, hata kama hakuna hofu ya kweli.

Gwaride la kijeshi lilijaa magari ya kijeshi ya Urusi yakihusisha vifaru vilivyotekwa ama kutelekezwa. 

Sherehe hizo zimefanyika bila shamra shamra zilizozoeleka huku maafisa wakionya kuwa Urusi inaweza kufanya mashambulizi ya makombora dhidi ya miji ya Ukraine.

Ikumbukwe, sherehe hizi huhusisha gwaride maalum la kumbukumbu la hatua ambazo Ukraine ilipitia kujipatia Uhuru wake.

“Ukraine ilizaliwa upya Februari 24 saa 4 asubuhi. Tulikuwa ni taifa ambalo halikulia, halikupiga mayowe, halikuogopa. Wananchi hawakuikimbia nchi yao, hawakukata tamaa. Hawatasahau,” amesema Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy  akirejea uvamizi wa kijeshi wa Urusi.