Shughuli ya uokozi katika ajali ya boti mbili zilizozama ndani ya Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 14 wilayani Bunda imekamilika baada ya miili yote kuopolewa.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema kazi hiyo imekamilika baada ya mwili wa 13 kuopolewa baada ya takriban siku nne za uokozi.
Kazi ya uokozi katika ajali hiyo imehusisha Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi na wavuvi wenye utaalam wa kupiga mbizi ambao wamefanya shughuli hiyo tangu jioni ya Julai 30, 2023 ajali ilipotokea.
Mwili wa mwisho umepatikana Saa 7:00 mchana wa leo Agosti 2, 2023 na hivyo kufikisha idadi ya watu 14 waliopoteza maisha katika ajali hiyo baada ya mwili wa mtoto kuopolewa siku ya kwanza ya ajali iliyohusisha waumini wa Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK) waliokuwa wanatoka kwenye ibada Kijiji cha Mchigondo.
Waumini hao wakiwemo watu wazima na watoto walikuwa wanaenda Kitongoji cha Bulomba Kijiji cha Igundu kabla ya boti zao zilizopakia abiria 14 kila moja kupigwa na dharuba na kuzama majini.
Watu 14 waliokolewa katika ajali hiyo iliyotokea saa 12:30 jioni ya Julai 30, 2023.
Miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyoacha simanzi katika vijiji vya Kata ya Igundu walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Bulomba wilayani Bunda.
Mkuu wa Mkoa Mara, Said Mtanda ameahidi kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi ya wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyoacha simanzi kwa wakazi wa vijiji vya Kata ya Igundu.
“Serikali italipigia gharama za kusafirisha miili ya wapendwa wetu kwenda sehemu ambayo familia itaamua kufanya mazishi pamoja na ubani wa Sh1 milioni kwa kila familia,” amesema