Miili minne kati ya mitano iliyokuwa imezama ndani ya Mto Mori wilayani Rorya baada ya mtumbiwi kuzama imepatikana baada ya miili mingine miwili kuopolea leo.
Idadi hiyo imefikiwa baada wazamiaji kufanikiwa kupata miili ya wanawake wawili jana jioni na miwili leo asubuhi kutokana na kazi ya utafutaji wa miili hiyo iliyoanza tangu kutokea kwa tukio la kuzama kwa mtumbwi Muliokuwa umebeba watu kumi ambapo watu watano walifariki huku watano wakinusurika.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema kuwa waopoaji hivi sasa wanaendelea na utafutaji wa mwili mmoja ambo ni wa mtoto wa miaka mitano.
Chikoka amesema kuwa ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza kutokea amezuia matumizi ya vivuko visivokuwa rasmi vilivyokuwa vikitumika kuvusha watu katika baadhi ya vijiji ambavyo mto huo umepita.
“Kuna vivuko visivyokuwa rasmi katika vijiji vitatu kikiwepo kijiji cha Kowak nimepiga marufuku matumizi ya vivuko hivyo kwasasa anayetaka kuvuka itabidi azunguke kwenye vivuko rasmi japokuwa kuna umbali lakini wananchi naomba watulewe kwani hii ni kwaajili ya usalama wao” amesema
Chikoka amesema kuwa baada miili yote kupatikana na mazishi kufanyika Serikali itatoa utaratibu rasmi wa namna ya kuvuka kwa usalama zaidi ili kuepuka matukio ya watu kuzama mtoni wakiwa wanavuka.
Amesema kuwa kabla ya kutoa utaratibu Serikali itakutana na wakazi wa vijiji hivyo na kujadiliana kisha kupanga utaratibu wa kuvuka mto kwa maelezo kuwa sio kila sehemu inafaa kutumika kama kivuko.
Mei 7, mtumbwi uliokuwa ukivusha watu kwenda katika kijiji cha Randa kata ya Kigunga kutoka kijiji cha Kowak ulizama maji na kuuwa watu watano.
Chanzo cha tukio hilo kimeelezwa kuwa ni kukatika kwa kamba iliyokuwa ikitumiwa na mvushaji kuvuta mtumbwi baada ya mtumbwi huo kubeba watu wengi kuliko uwezo wake huku kikitumia kamba ambazo pia zilikuwa zimechoka.