Mimba za Utotoni zinavyowatesa watoto kukwama kielimu Songwe

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael, ametoa muda wa siku tatu kwa Afisa elimu Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Jeshi la Polisi kuwasaka watu wote waliohusika kuwakatisha masomo wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari na kueleza hatua zilizochukuliwa kisha apewe taarifa.

Dkt. Francis ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya ugonjwa Malaria na uzinduzi wa mpango wa ugawaji wa vyandarua mkoani ambapo mkoa huo una kiwango cha chini cha maambukizi ya ugonjwa huo.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema hali ya maambukizi ya Malaria ni ndogo hivyo juhudi za Serikali kuendelea kupunguza maambukizi na kuhakikisha unatokomea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watu wanakuwa na matumizi sahihi ya vyandarua hasa watoto.

Amepiga marufuku tabia ya baadhinya watu kutumia vyandarua kufugia kuku na kuvulia samaki akionya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya hivyo kwakuwa ni kuihujumu Serikali na wadau wanaojitoa kupambana na maradhi hayo.

Akizungumzia takwimu zilizotolewa hivi karibuni hapa nchini, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis ameeleza kusikitika kwake kutokana na mkoa huo kuwa kinara kwa watoto kupata ujauzito.

“Ndugu zangu lakini kwenye utafiti kitaifa kuna jambo haliko sawa, RMO (Dkt. Bonifave Kasululu) ni jambo gani hilo ‘Ni kuongoza kwa watoto wanaopata mimba za mapema au mimba za utotoni’, sasa haiwezekani mkoa wetu (Songwe) kuongoza kwa mambo mabaya kama haya”, ameeleza Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Dkt. Francis amesema watoto kupata ujauzito wa mapema/mimba za utotoni ni kinyume cha sheria na kwamba ndio chanzo cha watoto kwenda kuolewa badala ya kujikita kwenye elimu huku ikichangiwa na baadhi ya wazazi na walezi wanaomalizana kinyemela kunapokuwa masuala hayo.

Kufuatia hayo, Mkuu huyo amemtaka Afisa elimu mkoa wa Songwe, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Songwe, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na wakurugenzi kwenda kushirikiana ili kuwabaini watoto wote walioacha masomo kwasababu ya mimba za mapema, watoto waliokatisha au kukatishwa masomo na kwenda kuolewa na watoto walioajiriwa katika kazi hatarishi jambo ambalo ni kinyume cha sheria pamoja kisha apewe taarifa kwa muda usiozidi siku tatu hatua zilizochukulia.

Mkuu huyo ameonyesha kukerwa na kitendo hicho ambapo ameelekeza wadau wote kushikamana kuhakikisha wanawalinda watoto ili watimize ndoto zao.

Amewataka pia wazazi na walezi kuachana na tamaduni zisizofaa za kutaka kuwaoza watoto ili wapate mali au kuwaweka kwenye uchungaji wa mifugo badala ya kuwapeleka na kuwasisitiza watoto kusoma kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

Katika kikao hicho Rc Dkt. Francis Michael, amezindua mpango wa ugawaji vyandarua na kwenda kutumika ipasavyo ili kuhakikisha mkoa huo unaendelea kupanda kwenye maambukizi madogo ya ugonjwa wa Malaria ikiwa ni pamoja na kudumisha usafi wa mazingira hasa kuwa na vyoo bora.

Amesema ni vema kila kaya ikawa na choo bora ili kuepuka magonjwa yanayoepukika kwani ndio dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuona wananchi wake wanakuwa na afya njema na kuwa chachu katika uzalishaji mali.