Miradi ya Maendeleo yatajwa kuwa chanzo cha ongezeko la deni la Taifa nchini Tanzania.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba

Serikali ya Tanzania, imesema ongezeko la deni la taifa linatokana na hatua yake ya kukopa fedha, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo inayofungua uchumi wa nchi.

Akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema deni hilo haliongezeki kwa sababu ya matumizi ya kawaida ya Serikali.

“Wala usiumize kichwa kutaka kujua limekopwa lini, sababu anayekopa si Rais, mnatafuta kitu kwenye kichaka ambacho sicho. You will never find it. Anayekopa sio Rais, inakopeshwa Serikali. Mikopo yote ya nchi yetu haikopeshwi kwa awamu,” amesema Dk. Mwigului.

Dk. Mwigulu amesema “hakuna mikopo inakopwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, mishahara au kwa ajili ya posho. Inakopwa kwa sababu ya miradi ya maendeleo inayofungua uchumi.”

Dk. Mwigulu ametaja miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa kwa kutumia fedha za mikopo, hasa ya barabara kwa kiwango cha lami, ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR).

“Kwa maana hiyo, mikopo ya bwawa imeshasainiwa sababu mradi unaendelea tutaendelea kupokea fedha zake. Mikopo ya SGR ilishakopwa tunaendelea kupokea sababu miradi yake inaendeleo,” amesema Dk. Mwigulu.

Waziri huyo wa fedha amesema, deni la Taifa ni himilivu, kwani uwiano wake na pato la taifa ni asilimia 31 kati ya asilimia 55 za ukomo wake, wakati na deni la nje kwa uwiano wa pato la taifa, ukiwa asilimia 18 kati ya 40 za ukomo wake.

Akizungumzia ulipaji wa madeni hayo, Dk. Mwigulu amesema “kuna madeni tumemalizia kulipa ya awamu ya kwanza, mimi mwenyewe nimesaini kulipa deni ambalo lilikopewa kabla sijazaliwa. Kuna madeni tunamalizia kulipa ya awamu ya pili, tatu na nne. Kuna madeni tunaendelea kulipa ya awamu ya tano na kuna madeni tunayoanza kulipa ya awamu hii.”