Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia Maria Matheo kwa tuhuma za kumuua mumewe, Gabriel Nguwa (80) kwa kumkaba shingo hadi kufa akiwa amelala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao aliwaambia waandishi wa habari jana mkoani hapa kwamba tukio hilo ni la Mei 30 mwaka huu saa 8:00 usiku, katika Kitongoji cha Bugweda, Kijiji cha Budushi, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa muda mrefu kati ya wanandoa hao hususani jioni mwanamke anapolewa na kuanza kumtuhumu mumewe kuwa hana msaada wowote katika maisha yao.
Abwao alisema kwamba mbinu iliyotumika ni kumvizia mume akiwa amelala na kumkaba shingoni na kusababisha kifo chake.
Katika hatua nyingine, mwezi uliopita jeshi hilo lilifanya msako na kuwakamata watu 71 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali.
Alisema katika makosa ya mauaji, walikamatwa watu 19, wizi watuhumiwa ni 31, uvunjaji ni watu 17 na watuhumiwa wanne wa makosa ya kubaka.
Aidha, jeshi hilo liliwakamata waganga wa kienyeji wawili wasiokuwa na vibali katika Kitongoji cha Lugange katika Kijiji cha Gilimba Kata ya Igulungu Wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Abwao aliwataja waganga hao kuwa ni Yunge Kija (25) na Bundi Makomango (29) ambao Mei 31 saa 3:00 asubuhi walikamatwa wakifanya shughuli za uganga wakiwa hawana vibali vya kazi hiyo