Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri na watumishi wengine kumi na tisa wa jiji hilo.
Watumishi hao wamesimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za serikali zaidi ya shilingi bilioni 10 zilizokusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa agizo hilo linatokana na matokeo ya ukaguzi maalumu kuhusu mapato ya ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Watumishi hao pia wamekabidhiwa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dar es Salaam kwa mahojiano.
Majaliwa alitoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wabunge, madiwani pamoja na watumishi wa Wilaya ya Ilala katika ukumbi wa Karimjee akiwa katika ziara yake ya kikazi Dar es Salaam.
Majaliwa alisema mbali na Shauri, watumishi wengine waliosimamishwa ni Tulusubya Kamalamo (Mweka Hazina), James Bangu (Mhasibu Mapato), Abdal- lah Mlwale (Mtunza Fedha Mkuu) na Mohammed Khais (Mhasibu wa Masoko).
Alisema watumishi hao wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo na hivyo kuisababishia halmashauri hasara ya shilingi 10,137,577,401 zilizokusanywa na mawakala na watumishi wa halmashauri hiyo lakini hazikuingizwa benki.
Pia, Majaliwa alitaja watumishi wengine wanao- paswa kuchukuliwa hatua kuwa ni Jesca Lugonzigwa (Ofisa Hesabu), Josephine Sandewa (Ofisa Hesabu), Tatu Mkangwa (kibarua) na Felician Maro (Mhasibu Msaidizi) ambao wameisababishia halmashauri hasara ya Sh 1,214,907,637.
Alitaja pia mawakala wanaodaiwa kufanya udanganyifu wa makusanyo ya mapato kwa kuchezea tarehe za PoS kwa kuzirudisha nyuma na hivyo makusanyo ya kiasi cha shilingi 131,356,400 kutoonekana kwenye taarifa za makusanyo.
Mawakala hao ni Pick Trading Ltd na Workers General Supply.
“Ripoti ya CAG imebaini kuwa wataalamu wa halmashauri waliohusika na upotevu wa mapato walikuwa wakiingilia moja kwa moja kati ya mfumo wa LGRCIS na benki na kuandika kwenye mfumo malipo ambayo hayakufika benki kwa lengo la kuficha ukweli wa kasoro na matumizi ya fedha kinyume cha sheria za fedha za umma.
Pia wahasibu waliingiza kwenye mfumo kiasi ambacho hakikupelekwa benki kwa lengo la kupotosha taarifa halisi za makusanyo,” alisema.
Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwepo kwa umakini kwenye ukusanyaji na matumizi ya mapato ili kuiwezesha serikali kuendelea kujenga miradi mingi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Uko mwenendo wa kutengeneza udanganyifu katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya halmashauri, kuna wakati wanaamua kuzima kwa saa mbili hadi tatu mfumo kwa kisingizio cha mtandao na mapato yatakayopatikana kwa muda huo hayafuati taratibu kwani badala ya kuyapeleka benki yanatumika kwa visingizio mbalimbali kama kulipa vibarua,” alisema.
Aliagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ufuatilie vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo na pia waweke makadirio ambayo yatawawezesha kukusanya zaidi.