Mkazi wa kijiji cha Dulisi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Hamisi Mayunga (27) amedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi kifuani na Mlinzi wa Kampuni ya Sam Security, Chacha Emmanuel, ambaye analinda ndani ya mgodi wa madini ya Almasi wa El-Hilali uliopo wilayani Kishapu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga George Kyando, akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, amesema tukio hilo limetokea Mei 20 mwaka huu majira ya saa 4 usiku.
Amesema marehemu Hamis Mayunga alikuwa na wenzake zaidi ya 10 wakivua samaki katika bwawa lililopo ndani ya mgodi huo wa El-Hilali, ndipo walinzi hao walipofika na kuwazuia kuvua, ndipo kukatokea kutoelewana na kusababisha mauaji.
“Wakati mzozo ukiendelea kwenye bwawa hilo ndipo mlinzi mmoja Emmanuel Chacha akiwa na wenzake wanne, akamfyatulia risasi na kumpiga kifuani upande wa kushoto na kufariki dunia papo hapo,” amesema Kyando.
Amesema baada ya tukio hilo mlinzi huyo alikimbia kusikojulikana, na kuitelekeza silaha aliyokuwa nayo aina ya Shortgun, na Jeshi hilo linamtafuta na akikamatwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Aidha, amesema jeshi hilo pia linawashikilia walinzi wenzake wanne, kwa ajili ya upelelezi zaidi juu ya tukio hilo, na kutoa wito kwa kampuni za ulinzi kuacha matumizi holela ya silaha, sababu hilo ni tukio la pili kutokea mkoani Shinyanga ndani ya mwezi mmoja walinzi kusababisha mauaji.