Mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola katika taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeenea hadi sehemu ya Kivu ya Kusini inayodhibitiwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, msemaji wa kundi hilo alithibitisha Alhamisi, na kuongeza hofu ya kusambaa zaidi kwa maradhi hayo.

Juhudi za kudhibiti mlipuko huu, ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa dharura ya kimataifa, zimekwamishwa na mizozo ya muda mrefu mashariki mwa DRC, ikiwemo mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23. Baada ya kuteka maeneo makubwa yenye utajiri wa madini kwa msaada wa Rwanda, M23 imeanzisha utawala sambamba na serikali ya Kongo. Hata hivyo, kundi hilo halijawahi kushughulikia janga kubwa la kiafya kama Ebola, ugonjwa ambao umesababisha vifo vya zaidi ya 15,000 barani Afrika katika kipindi cha nusu karne, na mlipuko wa sasa ukishahusishwa na vifo vya zaidi ya 130.
Kwa mujibu wa msemaji wa M23, vipimo vimethibitisha kisa kipya cha maambukizi kutoka Bukavu. Hakufafanua iwapo sampuli ilitoka ndani ya jiji hilo, lililotekwa na M23 Februari 2025, au maeneo ya vijijini yanayozunguka mji mkuu wa Kivu ya Kusini. Kisa hicho kilihusisha mtu mwenye umri wa miaka 28 kutoka Kisangani, mji mkubwa wa jimbo la Tshopo ambako hakuna maambukizi yaliyothibitishwa hadi sasa. “Mtu husika, rodha mwenzetu, alifariki kabla ya matokeo kuthibitishwa,” msemaji aliongeza, akisisitiza mazishi yalifanyika kwa kuzingatia kanuni za usalama. Mamlaka za Kongo bado hazijatoa kauli rasmi kuhusu kisa hicho.
Kwa mujibu wa WHO, mlipuko huu – wa 17 kuwahi kulikumba taifa lenye zaidi ya watu milioni 100 – unashukiwa kusababisha vifo 139 kati ya takribani 600 ya visa vinavyotiliwa shaka. Visa vingi vimeripotiwa katika Ituri, kitovu cha mlipuko, maeneo yenye vikundi vingi vya waasi. Maambukizi pia yamethibitishwa Kivu Kaskazini na Uganda, ambako mtu mmoja amefariki, lakini Kivu Kusini haikuwahi kuripotiwa hadi sasa. Changamoto za kufika maeneo yaliyoathirika zimefanya sampuli chache pekee kupimwa maabara, huku takwimu zikiegemea zaidi kwenye visa vinavyoshukiwa.
Kivu Kaskazini na Kusini zimegawanyika kwa mistari ya mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 pamoja na washirika wao wa Rwanda. Uwanja wa ndege wa Goma, uliokuwa ukirahisisha misaada ya dharura, umefungwa tangu M23 walipoteka mji huo Januari 2025. Hakuna chanjo wala tiba ya kitabibu kwa aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola vinavyosababisha mlipuko huu.
Raia wa Marekani aliyepata maambukizi akiwa DRC kwa sasa amelazwa hospitalini Ujerumani, huku mke na watoto wake watatu wakitengwa kwa maombi ya Washington. WHO imetathmini hatari ya mlipuko huu kuwa kubwa kwa DRC na ukanda wa Afrika ya Kati, lakini imesisitiza hatari ya janga la dunia nzima kuwa ndogo.
Marekani Jumatatu ilitangaza ukaguzi mkali kwa abiria wanaotoka DRC, Uganda na Sudan Kusini, huku Bahrain Jumanne ikipiga marufuku kwa mwezi mzima wageni kutoka nchi hizo tatu. Aidha, timu ya taifa ya mpira wa miguu ya DRC imefuta kambi ya mazoezi Kinshasa kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Mlipuko huu unajiri wakati mashirika ya kibinadamu yamepunguziwa bajeti, hususan kutokana na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani chini ya Rais Donald Trump. Moja ya hatua zake za mwanzo baada ya kurejea madarakani mwaka jana ilikuwa kuiondoa Marekani kutoka WHO, akililaumu shirika hilo kwa jinsi lilivyoshughulikia janga la Covid.