Shahidi wa pili wa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, John Mnyika, amemaliza kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama, akisisitiza kuwa baadhi ya mashtaka yaliyowahi kufunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho hayakuwa na msingi wa ushahidi.

Katika hatua ya mwisho ya ushahidi wake, Mnyika amesisitiza kuwa kauli yake kwamba kesi hizo zilikuwa za uongo ilitokana na kutokuwepo kwa ushahidi uliotosheleza kuthibitisha hatia. Akitoa ufafanuzi kuhusu kesi ya ugaidi iliyowahi kumkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mnyika amesema aliamini hakukuwa na mpango wa kufanya ugaidi na kwamba Mbowe alishtakiwa bila kuwa na hatia hiyo.
Mnyika pia ametoa ufafanuzi kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, harakati za CHADEMA za kudai mabadiliko ya uchaguzi, maana ya neno “uasi” na sababu zilizomfanya asipige kura. Amesema chama hicho kilikuwa kimejiandaa kushiriki uchaguzi, lakini kilitaka kwanza kufanyike marekebisho yatakayowezesha uchaguzi huru na wa haki.
Mnyika amesisitiza kuwa lengo la harakati hizo lilikuwa kuwaunganisha Watanzania na wadau wa haki hadi Serikali ikubali kufanya mabadiliko hayo.
Haya ni baadhi ya maswali na majibu yaliyotokea wakati Tundu Lissu, alipokuwa akimuuliza Mnyika maswali ya ufafanuzi baada ya kuhojiwa na upande wa Jamhuri:
LISSU: Umeulizwa kuhusiana na kifungu cha 7(1)cha sheria ya vyombo vya habari na ukaulizwa kama ni wajibu wa vyombo vya habari kutafuta habari, fafanua uliposema ni haki na uhuru wa vyombo vya habari kupata habari kwa uhuru wao.
Mnyika: Nilikua na maana kwamba vyombo vya habari vina uhuru wa kutafuta habari na kuchakata habari na kwenda kuchapisha habari hiyo.
LISSU: Unakumbuka ulisomeshwa Kamusi kuhusu neno Uasi, na ukaulizwa ukasema kwamba hiyo tafsiri ya neno Uasi sio tafsiri pekee ya neno Uasi, sasa naomba usome tena kisha ufafanue hilo jibu lako kwamba si tafsiri pekee.
Mnyika:Waheshimiwa majaji nilisema hivyo kwa sababu ukiangalia tafsiri B kwenye hii kamusi hii inaeleza kwamba ni vitendo vya kuipinga taasisi kwa hiyo si kuipinga Serikali pekee unaweza kuipinga taasisi au chama katika mazingira ya kisiasa.
LISSU:Sasa Umeulizwa maswali mengi sana juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na majibu yake haukuwa uchaguzi huru haki wala halali Waeleze Waheshimiwa majaji ulikuwa na maana gani.
Mnyika: Kwa sababu hakukua na mazingira ya watu kwenda kupiga kura kwa uhuru na matokeo kutangazwa kwa uhuru na haki kwa hiyo mfumo mzima wa uchaguzi haukua huru na haki.
LISSU:Unakumbuka uliulizwa juu ya ulichokisema kesi ya Ugaidi dhidi Mwenyekiti Mbowe na ukasema kesi hiyo ni uongo, ukaambiwa si alipatikana na kesi ya kujibu ukasema ndio lakini ni uongo ebu fafanua ulikua na maana gani kusema ni uongo.
Mnyika:Ni kwa sababu hakukua na hatia ya ugaidi na kumekuwa na tabia ya watu kubambikizia watu kesi na mahususi kwa Mwenyekiti Mbowe nafahamu kwamba hakuwa na mipango yoyote ya kufanya Ugaidi.
LISSU:Na shahidi kwenye suala hilo hilo uliulizwa kama ni kweli alishtakiwa pamoja na watu wengine ambao ni Makomandoo wa Jeshi na ukasema walikua ni makomandoo lakini wakati huo ni walinzi wake na walikua wanaharakati, ulikuwa na maana gani
Mnyika: walikua ni Makomandoo kwa maana waliwahi kulitumikia jeshi lakini walishaondoka na Mwenyekiti akawachukua kama walinzi wake na kwa kuwa walikua walinzi wake wakawa sehemu ya wanaharakati.
LISSU:Uliulizwa maswali juu ya vyombo vya ulinzi na swali lilikuwa kama unakubali au hukubali kwamba kutishia amani ni kutishia Rais na hivyo vyombo vya amani na jibu lako lilikuwa sio kila tisho lazima limlenge au hivyo vyombo
Mnyika:Kumtishia Rais au vyombo vya ulinzi inabidi hilo tishio lako la maneno au vitendo lazima liwalenge hao watu.
LISSU:Uliulizwa kama unajua Tanzania ni nchi huru ukajibu ndio, ukaulizwa kama ina Katiba yake ukajibu ndio, na ukaulizwa kama unajua kesi huamuliwa Kwa ushahidi halafu swali likawa kwanini unasema hizo kesi zoote ni za uongo na ukasema kesi zilifutwa kwa sababu zilikua za uongo, naomba ufafanuzi hapo.
Mnyika: Kesi zilikua za uongo kwa sababu hakukua na ushahidi mpaka Mahakama kufuta hatia na ndio maana nasema kesi zilikua za uongo.
LISSU:Uliulizwa maswali kuhusiana na mimi na wewe na Sugu kukamatwa Mbeya tarehe 11 Agosti 2024 na ukaeleza kwamba mimi nilipokamatwa nilipelekwa sehemu isiyojulikana kwanini ulisema sehemu isiyojulikana
Mnyika:Siku hiyo ya tarehe 11 Agosti 2024, ulipochukuliwa mbele yangu Kamanda Awadh ambaye alikua kiongozi wa Operesheni na RPC wa Mbeya hawakutaka kusema wanakupeleka wapi
LISSU:Shahidi uliulizwa kuhusiana na hotuba yangu na swali lilikuwa ueleze kama ni sahihi au si sahihi kwamba lengo kuishinikiza Serikali ili yapatikane hayo mabadiliko ukasema hapana hilo halikua lengo naomba ufafanue
Mnyika: Lengo lilikuwa ni kuwaunganisha Watanzania na Wadau wote wa Haki mpaka Serikali ikubali kufanya mabadiliko yatayopelekea uchaguzi huru na haki
LISSU:Uliulizwa kwamba ni sahihi au si sahihi kwamba harakati hizo za kudai mabadiliko ziliendelea hata baada ya mimi kukamatwa na jibu lako ukasema hapana ukasema ziliendelea mpaka tarehe 9 Juni 2025, naomba ufafanue
Mnyika:Nilikua na maana kwamba tarehe 10 Juni 2025, Mahakama ilitoa zuio dhidi ya Chadema, kutumia mali zozote Za chama, mikutano ya hadhar ilikua inaendelea ikazuiwa kwa hiyo shughuli zote za siasa zilisimama mpka trh 10 Aprli lilipoondolewa na Mahakama ya Rufaa
LISSU:Uliulizwa sana kama kuhamasisha Uasi ni njia ya Kidemokrasia ya kutaka mabadiliko na ukajibu kwamba ni njia ya Kidemokrasia naomba ufafanuzi.
Mnyika: Uasi ni kupinga au kukataa kwa nguvu kubwa na kufanya kwa njia za Kidemokrasia kwa kutumia haki za kisiasa zilizopo kwenye sheria ya vyama vya siasa na Katiba ya nchi na mikataba ya Kimataifa ambayo nchi yetu imesaini
LISSU:Uliulizwa kama Chama chako kilikuwa kimejiandaa kushiriki uchaguzi kwa Katiba iliyopo na jibu lako ukasema kilijiandaa kwa katiba iliyopo na marekebisho tuliomba yafanyike, naomba ufafanue ulikua na maana gani?
Mnyika:Tulijiandaa kwa maana ya kufungua milango kwa watia nia wa uchaguzi kujitokeza kuandika kusudio la kugombea kwao na tulijiandaa kwa kuendesha program za mafunzo ya chama kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi kwa hiyo tulijiandaa na uchaguzi
LISSU:Sasa Shahidi kuna mahali uliulizwa kwamba unakubaliana nae kwamba kuhamasisha uasi ni kosa ukasema Mwalimu Nyerere alisema tunataka Vijana waasi dhidi ya Ukandamizi ulikua na maana gani
Mnyika: Nilikua na maana kwamba Uasi yana tafsiri ya ziada iliyotumika na Mwl Nyerere kwa maana ya Uasi dhidi ya ukandamizaji
LISSU:Shahidi uliulizwa kama ni kweli kwamba chama chako kilipata fursa ya kupata kutoa maoni ya Katiba ukasema ndio lakini kwa sababu yalikataliwa mbele ya Tume ya Katiba
Mnyika:Waheshimiwa Majaji maoni yote tuliyokuwa tunazungumza ya kurekebisha Katiba kuwezesha uchaguzi huru na haki mathalani kupinga Matokeo ya Urais Mahakamani , kuundwa tume huru ya uchaguzi kipaza sauti kilikuwa kinazimwa kila ilipokuwa unataja Katiba na unaambiwa maoni hayo hayapokelwei
LISSU:Uliulizwa kama ulipiga kura ukasema hapana hukupiga kura kwa sababu hakukua na uchaguzi ulikuwa na maana gani?
Mnyika:Nilikua na maana ya kwamba hakukua na uchaguzi huru, haki na halali kwa hiyo hakukua na sababu ya mimi kwenda kwenye uchaguzi
Kesi Inaendelea