Mrithi wa Maalim Seif kupatikana kesho

Halmashauri Kuu ya chama cha ACT Wazalendo imepitisha majina ya wagombea wa nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.

Waliopitishwa kwa nafasi ya mwenyekiti ni Juma Duni Haji na Hamad Masoud Hamad huku upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti, amepitishwa Othman Masoud Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Juma Said Saanane.

Akizungumza na wanahabari leo Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Salim Bimani amesema wagombea hao watachuana kwenye uchaguzi utakaofanyika kesho kwenye mkutano mkuu wa chama hicho.

“Halmashauri kuu ilipokea mapendekezo ya wagombea kutoka kamati kuu iliyokaa jana na baada ya kuyachambua, imepitisha majina ya wagombea hawa ambao kesho ndiyo watashiriki kwenye uchaguzi,” amesema Bimani..

Kwa upande wa nafasi ya mjumbe wa Kamati Kuu, Bimani amesema halmashauri kuu imepitisha majina mawili kati ya saba waliojitokeza kujaza nafasi hiyo kwa upande wa Tanzania Bara.

“Chama chetu kimeendesha mchakato huu kwa haki na kwa kufuata demokrasia. Tulitangaza Januari 4 – 17 kuwa tarehe za kuchukua fomu, watu walijitokeza na sekretarieti ilipitia wagombea wote na kuwasilisha ngazi za juu,” amesema Bimani.

https://mwanzotv.com/2022/01/19/nani-kumrithi-maalim-seif-sharif-hamad/

Nafasi ya mwenyekiti ilikuwa inashikiliwa na Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17 mwaka jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alipokuwa akipatiwa matibabu

Kesho ndiyo siku ambayo atapatikana mrithi wa Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho.