Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Kinondoni imekubali maombi ya upande wa waleta maombi, katika kesi iliyofunguliwa dhidi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, kutafutwa kwenye makazi yake ya Dar es Salaam na kijijini kwao Koromije Misungwi mkoani Mwanza.
Wakili wa upande wa waleta maombi Nyaronyo Kicheere, ameeleza kwamba wameshindwa kumpata mjibu maombi namba 3 ambaye ni Paul Christian Makonda kwa kuwa Masaki alikokuwa anakaa amekwishahama na namba yake ya simu haipatikani na hivyo kuiomba Mahakama hiyo iwapatie hati ya kumsaka maeneo mbalimbali.
Aidha wameomba kupewa hati za wito ambazo zitapelekwa alipokuwa akifanyia kazi kwa mara ya mwisho, kwenye nyumba aliyokuwa anaishi kwa mara ya mwisho, maeneo anayotembelea mara kwa mara na nyingine iwekwe katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, nyingine ipelekwe bandarini, Kolomije, Misungwi mkoani Mwanza na ya mwisho ipelekwe kwenye gazeti la Kiswahili na la kingereza.
Wakili Nyaronyo, ameongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kutaka mjibu maombi hayo ambaye ni Paul Makonda apate taarifa juu ya uwepo wa kesi hiyo mahakamani.
Kwa upande wake Hakimu wa mahakama hiyo Aron Ryamuya, ameeleza kuwa hoja ya kwenda kubandika hati hizo katika viwanja vya ndege na bandarini ni kinyume cha sheria na ni uchafuzi wa mazingira na badala yake akakubali matangazo hayo yapelekwe kwenye nyumba yake ya Masaki aliyokuwa akiishi, kwenye gazeti na kijijini kwao Koromije pekee.
Kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2022, imeahirishwa hadi Machi 2, 2022.