Mshtakiwa azimia mahakamani kesi ya Zumaridi

Kesi ya Jinai namba 12/2022 imeshindwa kuendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza baada ya mshtakiwa namba 38 kudondoka ghafla mahakamani na kuzimia dakika chache kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Katika kesi hiyo Diana Bundala maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi’ na wenzake 84 wanakabiliwa na shtaka la kufanya kusanyiko lisilo na kibali.

Tukio la mshtakiwa huyo namba 38, Mariam Julius kudondoka mahakamani lilitokea leo Septemba 19, 2022 asubuhi baada ya mshtakiwa huyo kuanza kupiga kelele kisha kudondoka na kuanza kutoa mapovu mdomoni.

Baada ya mshtakiwa huyo kutolewa nje, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Clescensia Mushi ambaye anasikiliza kesi hiyo akaingia ndani ya chumba cha mahakama na kuuliza jopo la mawakili wa pande zote iwapo wako tayari kuendelea na shauri hilo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dorcas Akyoo ameieleza mahakama kuwa upande wa jamhuri uko tayari kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa yenye lengo la kuondoa utata wa saini iliyotiliwa mashaka kwenye maelezo ya onyo ya mshtakiwa namba moja, Diana Bundala aliyedai saini hiyo siyo ya kwake.

“Tuko tayari kuendelea na tumeleta shahidi mmoja kwa ajili ya kutoa ushahidi wake kwenye kesi ndogo ndani ya kesi kubwa iliyoibuliwa katika shauri hili,” ameeleza Akyoo

Hata hivyo, kabla ya kuendelea, wakili wa utetezi, Linus Amri alisimama kwa niaba ya jopo la mawakili wa utetezi na kuiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi pale mshtakiwa atakaporejea kwenye utimamu wa afya yake.

“Tulikuwa tayari kuendelea lakini kuna changamoto ambayo imejitokeza kwa mshtakiwa namba 38 ambaye amepata ugonjwa wa ghafla na kwa upande wetu hatuoni kama ni jambo la busara kuendelea akiwa hayupo mahakamani,” ameeleza Amri

Baada ya hoja za pande zote, Hakimu, Clescensia Mushi ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumanne Saa 3:30 asubuhi itakapoitwa kwa ajili ya usikilizaji wa ushahidi wa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa.

Chanzo Mwananchi