Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na vilio vya bei ya mafuta katika ziara yake ya siku nne mkoani Mbeya, huku akiahidi kuwa serikali ya nchi hiyo ipo macho na inajitahidi bei isipande kama zilivyo baadhi ya nchi.
Mapema wiki hii Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), ilitangaza bei mpya za ukomo wa mafuta, ikionesha Jiji la Dar es Salaam lita moja ya petroli ni shilingi 3,410 na shilingi 3,322 kwa dizeli, huku mafuta ya taa yakifika shilingi 3,765.
Rais Samia akizungumzia vilio vya wananchi leo Agosti 5, 2022 Mbalizi mkoani Mbeya, amesema mafuta ya kula na ya gari yalikuwa yameadimika, lakini serikali tayari imepatia ufumbuzi mafuta ya kula na kuleta unafuu wa bei, hata hivyo amekiri kuwa mafuta ya gari bado ni changamoto kubwa kutokana na kupanda zaidi kwenye soko la dunia kunakusababishwa na vita ya Ukraine na Urusi.
“ Serikali inatoa shilingi bilioni 100 kila mwezi, ili bei zibaki hivyo zilivyo, tukiacha bei ya dunia itakuwa ghali sana, mafuta ni duniani kote mpaka waache kupigana, ndio tutarudi kuwa sawa,”amesema Rais Samia na kuongeza:
“Ndugu zangu kwenye mafuta serikali tupo macho, tunajitaidi kufanya bei isipande zaidi kama wenzetu. Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki kuna nchi mafuta hayanunuliki…
“Tatizo la mafuta ni la dunia nzima, serikali bado tunaendelea kuangalia, isingekuwa hivyo shilingi bilioni 100 zingeingizwa kwenye miradi ya maendeleo.”
Amesema bei ya mafuta inaendelea kupanda duniani, “lakini sisi tunashusha kwa kutoa ruzuku na Serikali ipo macho tunafanya kuhakikisha bei isipande kiasi kile kilichopanda kwa wenzetu.”
Amesema kwenye nchi zingine za Afrika Mashariki mafuta “hayanunuliki, lakini marais wote tunajitahidi kwa njia yeyote kila mmojakwa namna yake kupunguza bei ya mafuta, bei ya mafuta ni tatizo la ulimwengu mzima tunajitahidi bei zibakie pale zilipo kwa hiyo kuhusu mafuta Serikali yenu tunahangaika.”
Bei ya mafuta imepanda tena mwezi huu na kuivuka ile ya Julai 2022, ambapo petroli imepanda kwa shilingi 190 kwa kila lita na shilingi 179 kwa kila lita ya dizeli huku mafuta ya taa yakipanda kwa shilingi 323 kwa kila lita katika jiji la Dar es Salaam.
Kwa mkoa wa Mbeya bei ya petroli ni shilingi 3,533, dizeli shilingi 3,445 na mafuta ya taa shilingi 3,888 ikiwa ni bei baada ya ruzuku.