Mkutano wa 14 wa Bunge la 12 umeanza leo ambapo unatarajiwa kufanyika kwa muda wa wiki tatu kuanzia leo tarehe 30 Januari hadi tarehe 16 Februari 2024, huku hoja kubwa ikiwa mjadala wa miswada mitatu iliyowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba mwaka jana.
Miswada hiyo ambayo imeibua mjadala pamoja na kupingwa na wadau mbalimbali ikiwamo vyama vya siasa, imetajwa kuwa na uzito wa kipekee kiasi cha kuongezewa muda wa wiki moja tofauti na utaratibu wa kawaida wa bunge kukaa wiki mbili.
Mapema leo asubuhi miswada hiyo ilisomwa huku Serikali ikiwa na mapendekezo yaliyotolewa na wadau katika nyanja tofauti, hata hivyo mapendekezo hayo yameonekana kuwa tofauti na maoni ya Kamati Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.
Awali akisoma mswada huo kwa mara ya pili bungeni, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge na Uratibu, Jenister Mhagama amesema sheria inayopendekezwa katika muswada wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani unakusudia kuunganisha sheria mbili zinazohusiana na masuala ya chaguzi.
Sheria hizo ni sheria ya uchaguzi sura ya 343 na sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa, sura ya 292 ambapo waziri Mhagama amesema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba masharti ya sheria hizo mbili za uchaguzi yanafanana.
Aidha hoja ya kutaka wakurugenzi wa halmashauri (DED) waendelee kusimamia uchaguzi imewekewa mkazo jambo lililozidi kuwavuruga wadau wa demokrasia kuona kwamba hoja zao hazikuwekewa maanani.
Hata hivyo mara baada ya wasilisho la Mswada huo, taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Joseph Mhagama ilieleza kamati ina maoni kwamba sheria isiweke ulazima kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kusimamia uchaguzi.
Badala yake, imeshauri kuwepo na masharti ya mtumishi wa umma mwandamizi ama mtu mwingine yoyote mwenye sifa kuteuliwa kuwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi.
Kamati hiyo imesema Serikali iliona upo umuhimu wa wakurugenzi watendaji kutajwa kwenye sheria kwa kuwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu ziliona hazikiuki masharti ya Katiba.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, inaona hakuna ulazima wa sheria kuweka sharti kwa mkurugenzi wa jiji, manispaa, mji na wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi au wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kama kifungu hicho cha 6 (1) kinavyoeleza.
Kamati hiyo imesema hiyo ni kwa kuwa uzoefu unaonyesha wapo wakurugenzi kwa sababu mbalimbali wanapoteza sifa za kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Kamati hiyo ikalieleza Bunge imeandaa jedwali la marekebisho ya kamati ya kuwatumia watumishi wa umma waandamizi ama mtu yoyote mwenye sifa kwa lengo la kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata.
Miswada ambayo imepangwa kujadiliwa katika mkutano huo ni Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023.
Miswada mingine ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 na muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023.
Wadau wadai maoni yao kutowekewa maanani
Hata hivyo, wadau walikuwa na matumaini muswada huo wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2023, ungezingatia maoni yao juu ya swala hilo, lakini uliposomwa kwa mara ya kwanza, hakukuwa na mabadiliko.
Walikwenda mbali zaidi wakitaka miswada hiyo iondolewa bungeni ili kurudiwa upya kwa maoni kwani kwa sasa miswada hiyo ni mibovu
Kupitia ukurasa wake wa X (Twitter) Leo Jumanne, Januari 30, 2024 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameandika kuwa maoni yao na ya wadau yamepuuzwa na kueleza kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, miswada hiyo aliyodai ni mibovu utajadiliwa.
“Maoni yetu na ya wadau yamepuuzwa, kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa kwenye tovuti ya miswada mibovu ya uchaguzi na vyama itajadiliwa kuanzia leo mpaka tarehe 2 Februari 2024. Tafsiri rahisi ni kuwa inakwenda kupitishwa bila kuanza na mabadiliko au marekebisho ya katiba” ameandika Mnyika.