Mtalii mmoja mwenye asili ya China afariki kwa ajali katika Hifadhi ya Serengeti

Mtalii mmoja amefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) leo Julai 29, 2024 gari hiyo ilikuwa na watalii saba wenye asili ya China na dereva raia wa Tanzania.

“Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) linapenda kuutaarifu umma kuwa jana  saa 10 jioni gari la watalii lenye namba za usajili T603 DCL mali ya Kampuni ya Yonda Africa lilipata ajali likiwa njiani kurudi hotelini kilomita moja kutoka Lobo Wildlife Lodge katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mugumu na majeruhi sita wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Pia, Tanapa wamesema uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.