Mtoto wa miaka 15 jina linahifadhiwa anayeishi Kihesa Manispaa ya Iringa amedaiwa kuwabaka na kuwalawiti jumla ya watoto 19 katika kipindi cha miaka minne.
Mtoto huyo amebainika jana Machi 14, baada ya Dawati la Jinsia la Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usitawi wa jamii wa Manispaa na Mkoa huo kufanya oparesheni ya kuwasaka watuhumiwa wa matukio ya udhalilishaji.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igeleke, Sigfriend Mapunda alisema kuwa alimbaini mtoto mmoja darasani baada ya kuona anatoa harufu na kumhoji na kutaja watoto wengine waliokuwa wakifanyiwa vitendo hivyo.
“Nilimgundua mtoto mmoja baada ya mtoto mwenzie kuja kushtaki kwangu nikamuita nikamuhoji akakiri na kuwataja wenzake na wengine wengi hadi kufikia idadi ya watoto 19.” Amesema mwalimu huyo na kuongeza kuwa
“Mtoto mwingine nilimuona ananuka anatoa harufu mbaya nikamuhoji na kukiri kufanyiwa kitendo cha udhalilishaji na kijana mwenye umri wa miaka 15 ambapo mtoto huyo aliwataja watoto wengine ambao wanafanyiwa vitendo hivyo,” amesema.
Amesema baada ya kuwabaini watoto hao, aliwapigia simu wazazi wao badaye kwenda kuripoti tukio hilo polisi na kuwapeleka hospitali ambako walithibitika kufanyiwa vitendo hivyo.
“Tunawaomba wazazi wawe karibu na watoto wao wasiwaache watoto wakarubuniwa kwa kuangalia TV na vizawadi vidogo vidogo wawe marafiki wa watoto wao ili linapotokea tatizo waweze kuwaelezea na kulichukulia hatua” amesema
Mmoja wa wazazi mwenye mtoto aliyefanyiwa ukatili amesema aligundua mtoto wake amefanyiwa vitendo hivyo wakati akimuogesha.
“Niligundua mtoto wangu wa kike kafanyiwa vitendo vya uzalilishaji wakati namuogesha akasema anasikia maumivu sehemu za siri ndio nikamuuliza akaniambia kilichotokea nikaamua kwenda kushitaki polisi na tukaenda kupima hospitali ikathibitika ni kweli ameingiliwa,” amesema.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai amesema kutokana na ongezeko la ubakaji na ulawiti wa watoto mkoani humo, wameamua kufanya kampeni ya kupinga ukatili kwa watoto ili kunusuru watoto na kuondoka na janga hilo.
“Cha kusikitisha zaidi mtuhumiwa wa tukio hili ni mtoto, hivyo tumemuweka chini ya ulinzi wa Polisi ili kumlinda na hasira za wananchi wenye hasira kali baada ya kuona watoto wa wahanga wanasema kwa kuwa ni mtoto lazima tutamuachia hivyo atabaki na sisi polisi mpaka pale taratibu zingine zitakapofuata,” amesema.
Kwa mujibu wa Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa huo, Sauda Mgeni vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka 2019 waliripotiwa watoto 404, mwaka 2020 watoto 439 na mwaka 2021 watoto 384 kwa mujibu wa watoto waliripotiwa polisi kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti.