Donald Trump Jr ambaye ni mtoto mkubwa wa kiume wa Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump, yupo nchini Tanzania kutembelea maeneo mbalimbali huku kueleza kuvutiwa na vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Akiwa nchini, Trump Junior amefanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa na kuelezwa fursa za utalii zilizopo nchini.
Waziri Mchengerwa alimuomba mtoto huyo wa Trump kuendelea kuwa balozi wa Utalii wa Tanzania kwani imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine.
Waziri Mchengerwa alimweleza mgeni huyo mashuhuri mwelekeo wa sekta ya utalii na fursa mbalimbali za uwekezaji.
“Tanzania tuna mwelekeo mzuri katika kukuza utalii na kuvutia watalii zaidi, kwa kuboreshwa huduma za utalii ikiwepo miundombinu ya hifadhini,” amesema.
Kwa upande wake Trump Junior ambaye pia ni mfanyabiashara mkubwa nchini Marekani na Makamu wa Rais Mwandamizi katika kampuni kubwa ya baba yake, huku akitajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola Milioni 350 (zaidi ya Shilingi Bilioni 750), ameeleza kufurahishwa na Tanzania.
Trump ameahidi kutembelea maeneo mbalimbali zaidi ikiwemo eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na hifadhi nyingine.