Mtu mmoja afariki dunia huku wengine saba wakijeruhiwa kwa mlipuko wa baruti

Mtu mmoja amefariki dunia na saba wamejeruhiwa kufuatia mlipuko wa baruti uliotokea jana tarehe 01.07.2026 majira ya saa 12:46 asubuhi kwenye kibanda cha kahawa katika Mtaa wa Sahwa ya Juu, Kata ya Lwanhima, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Akielezea chanzo cha tukio hilo Kamanda amewataja kwa majina watu waliojereuhiwa katika tukio hilo kuwa ni Daudi Joseph Baraka (54), Muuza kahawa na mkazi wa Sahwa, Emmanuel Luhangwa Joseph (40), Fundi ujenzi na mkazi wa Sahwa, Yusufu Rajabu Nasoro (20), Fundi ujenzi na mkazi wa Sahwa na ​Zawadi Saimon Ndukeji (27) , Mama lishe na mkazi wa Sahwa Juu.

Wengine ni ​James Hussein Ntugo (33) , Fundi ujenzi na mkazi wa Sahwa Juu, Joseph Muyagingwa Englibert (22), Fundi ujenzi na mkazi wa Sahwa na Marco Mahunge Chandanoba (45), Mpasua mawe na mkazi wa Igwambiti “A”.

Aidha Kamanda Mutafungwa amesema chanzo cha mlipuko huo ni uzembe wa utunzaji wa baruti kwani  Marehemu alibeba baruti hizo na kukaa nazo karibu na jiko la mkaa lililokuwa linawaka kwenye kibanda hicho cha kahawa huku akifahamu wazi kuwa baruti hizo zikipata joto hulipuka.

Eneo la tukio limeshakaguliwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wataalamu wengine, wakiwemo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na maafisa kutoka Tume ya Madini Mwanza na wamejiridhisha kuwa lipo salama kwa matumizi ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu watu wanaotumia na kumiliki baruti pasipo kuwa na kibali huku akiwataka wenyeviti wa mitaa kufanya ukaguzi ili kuwabaini watu hao katika mitaa yao.

​Naye, afisa kutoka Tume ya Madini Mkoa wa  Mwanza, Deus Makuli, amesema ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kumiliki baruti bila kuwa na leseni na kusema kuwa marehemu alikuwa akimiliki baruti hizo bila kuwa na vibali.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za mitaa kuhakikisha watu hawafanyi shughuli za kuripua mawe bila kuwa na vibali na wakiwabaini watoe taarifa kwa vyombo husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Baadhi ya wananchi, akiwemo Mahuma Mungu na Adili Atare ambao ni wakazi wa Lwanhima, wameeleza kusikitishwa na tukio hilo na wameahidi kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wanaotumia vilipuzi kwa ajili ya kulipua mawe katika maeneo yao bila kuwa na vibali halali ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Majeruhi katika ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba) na mmoja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi.